Osimhen apiga hat trick, Galatasaray ikiizamisha Ajax
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Nigeria, amefikisha jumla ya mabao sita katika mashindano ya Ulaya msimu huu baada ya usiku wa Novemba 5, 2025 kufunga bao la kwanza dakika ya 59, kisha kuongeza mawili kupitia mikwaju ya penalti.
AMSTERDAM, UHOLANZI: Victor Osimhen amefunga hat-trick wakati Galatasaray ikiipa Ajax kipigo cha nne mfululizo kwa matokeo ya 0-3 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, mechi ikipigwa Johan Cruijff Arena.
Mshambuliaji huyo wa Nigeria, amefikisha jumla ya mabao sita katika mashindano ya Ulaya msimu huu baada ya usiku wa Novemba 5, 2025 kufunga bao la kwanza dakika ya 59, kisha kuongeza mawili kupitia mikwaju ya penalti.
Kwa hat-trick hiyo, Osimhen amefikisha mabao 25 kwenye michuano ya Ulaya na kumbwaga aliyekuwa mshambuliaji wa Inter Milan na Newcastle, Obafemi Martins, kuwa mfungaji bora wa Nigeria wa muda wote barani Ulaya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ndiye kinara wa mabao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, akitangulia kwa bao moja mbele ya Harry Kane, Erling Haaland na Kylian Mbappe.
Ajax ilienda mapumziko bila kufungwa, ikimshukuru kipa wao, Remko Pasveer aliyefanya maajabu kwa kuokoa mipira miwili ya hatari kutoka kwa Osimhen.
Hata hivyo, Pasveer hakuweza kumzuia mshambuliaji huyo baada ya kipindi cha pili kuanza, ambapo Osimhen alitangulia mbele ya beki Josip Sutalo na kuunganisha kwa kichwa krosi ya Leroy Sane.
Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa Ajax baada ya mwamuzi kuwapa wenyeji penalti mbili, zote zikitokana na makosa ya kugusa mpira kwa mkono.
Osimhen alifunga kwa urahisi penalti ya kwanza, baada ya ukaguzi wa VAR kuonyesha mpira ulimgonga mguuni Youri Baas kisha ukapiga mkono wake.
Hakukosea pia kwa penalti ya pili, iliyotolewa baada ya kosa la Anton Gaaei, ambapo alifyatua mkwaju mkali uliokwenda moja kwa moja kwenye kona ya juu kulia.
Matokeo hayo yanaiacha Ajax ikiburuza mkia kwenye kundi, ikiwa imepoteza mechi zote nne za Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 14–1.
Wakati huo huo, Galatasaray imepanda hadi nafasi ya tisa na kusogea karibu na nafasi ya nane bora, ambapo timu zinapata tiketi ya moja kwa moja ya kufuzu hatua ya mtoano.