Bondia afariki baada ya miaka 11 ya kupambania uhai
Muktasari:
- Colón alikuwa ameishi kwa takribani miaka 11 akiwa na ulemavu mkubwa wa ubongo baada ya kupata jeraha baya katika pambano lake dhidi ya Terrell Williams Oktoba 17, 2015, huko Virginia, Marekani.
BONDIA maarufu wa Puerto Rico, Prichard Colón, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 33, Alhamisi ya Agosti 13, 2026. Kifo chake kimethibitishwa na baba yake, Richard Colón, kupitia mitandao ya kijamii.
Colón alikuwa ameishi kwa takribani miaka 11 akiwa na ulemavu mkubwa wa ubongo baada ya kupata jeraha baya katika pambano lake dhidi ya Terrell Williams Oktoba 17, 2015, huko Virginia, Marekani.
Wakati wa pambano hilo, Colón alipigwa mara kadhaa ngumi nyuma ya kichwa, maarufu kama rabbit punches. Baada ya pambano kumalizika, Colón alirejea chumba cha kubadilishia nguo, akaanza kutapika na baadaye akaanguka.
Madaktari walibaini kuwa alikuwa amepata uvujaji mkubwa wa damu kwenye ubongo, hali iliyomlazimu kufanyiwa upasuaji wa dharura. Baadaye alikaa kwenye koma kwa siku 221 ambapo ni zaidi ya miezi saba.
Alipozinduka, maisha yake yalibadilika kabisa. Colón alipoteza uwezo wa kutembea, kuzungumza na kujihudumia, kwa miaka iliyofuata alihitaji uangalizi wa karibu wa wazazi wake.
Kabla ya tukio hilo, Colón alikuwa akitabiriwa kuwa nyota mkubwa wa dunia ya ngumi. Akiwa na umri wa miaka 23, alikuwa hajapoteza pambano lolote, akiwa na rekodi ya ushindi 16, ikiwemo KO 13.
Mwaka 2021, WBC ilimtunuku heshima ya kuwa “Bingwa wa Heshima wa Dunia” kutokana na safari yake na mchango wake katika mchezo wa ngumi.
Kifo cha Prichard Colón kimeacha huzuni kubwa kwa mashabiki wa ngumi duniani, huku simulizi ya maisha yake ikiwa ukumbusho wa hatari kubwa ambazo mabondia hukabiliana nazo ndani ya ulingo.