Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hakuna kulala, Ulaya yachangamka

ULAYA Pict

Muktasari:

  • Nchini Hispania 'LaLiga' inaanza leo, huku Ligue 1, Serie A na Bundesliga zikifuata hivi karibuni, katika msimu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

LONDON, ENGLAND: WAKATI Ligi Kuu England ikiwa imebakiza wiki moja kuanza, ligi nyingine kubwa barani Ulaya tayari zinaanza kutimua vumbi msimu huu.

Nchini Hispania 'LaLiga' inaanza leo, huku Ligue 1, Serie A na Bundesliga zikifuata hivi karibuni, katika msimu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.


ULA 01

LALIGA: MOURINHO AREJEA REAL MADRID

Mchezo wa kwanza: Alaves v Getafe, Leo,Jumamosi, Agosti 15.

Kocha Jose Mourinho kurejea Real Madrid baada ya miaka 13 kupita tangu alipomaliza kipindi chake cha kwanza cha kuinoa klabu hiyo ni jambo ambalo wengi hawakulitarajia.

Wengi walitarajia Real Madrid kutawala LaLiga na Ligi ya Mabingwa baada ya kumsajili Kylian Mbappe mwaka 2024. Ingawa Mbappe ameonyesha kiwango kizuri, timu kwa ujumla haijaonekana kuungana ipasavyo.

Msimu uliopita, Real Madrid ilionekana kama timu mbili tofauti ndani ya uwanja; kundi la washambuliaji nyota wanne na safu dhaifu ya ulinzi iliyokuwa ikiacha nafasi kwa wapinzani kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Usajili wa Marc Cucurella, Ibrahima Konate, Denzel Dumfries na Bernardo Silva unatarajiwa kuimarisha ulinzi, huku Yan Diomande akitarajiwa kuongeza ubunifu katika eneo la mwisho la mashambulizi.

Mshambuliaji Vinicius Junior  amesaini mkataba mpya baada ya awali kuhusishwa na Arsenal.

Mourinho ni kocha mwenye uzoefu mkubwa, anakabiliwa na swali kubwa kadhaa kama bado ana uwezo wa kuongoza kikosi chenye mastaa kama Mbappe, Jude Bellingham na Vinicius.

Pia, kuna swali la kama ataweza kudhibiti masuala ya ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, jambo ambalo lilimwandama katika kipindi chake cha kwanza Bernabeu, pamoja na kama bado ana mbinu za kutosha za kuipiku Barcelona.

Barcelona ya Hansi Flick haikuwa na nguvu kama ilivyokuwa msimu wa 2024/25, lakini ikiwa na kikosi kilichojaa wachezaji wa Hispania walioshinda Kombe la Dunia, bado inaonekana kuwa kinara wa kuwania taji la LaLiga kwa mara ya tatu mfululizo.

Kuziba pengo la mshambuliaji Robert Lewandowski haitakuwa kazi rahisi, lakini Barcelona imeongeza nguvu kwa kuwasajili Anthony Gordon na Karim Adeyemi.

Kama kawaida, Atletico Madrid itajaribu kuingia katika nafasi mbili za juu, huku Villarreal na Real Betis zikitarajiwa kuwania nafasi za juu baada ya vigogo hao.

Malaga, ambayo imepanda kutoka daraja la tatu, itajaribu kujinusuru na kushuka daraja ikiwa na kikosi chenye bajeti ndogo, lakini mshikamano mkubwa. Klabu hiyo imekuwa chini ya usimamizi wa mahakama tangu mwaka 2020.

Kwa upande mwingine, Valencia itacheza msimu wake wa mwisho katika Uwanja maarufu wa Mestalla kabla ya kuhamia uwanja mwingine.

Rayo Vallecano nayo iko kwenye sintofahamu kuhusu matumizi ya Uwanja wa Vallecas baada ya serikali ya eneo la Madrid kuiondolea klabu hiyo leseni ya kuandaa mechi kutokana na hali mbaya ya miundombinu ya uwanja huo.


ULA 02

SERIE A: MAKOCHA WAPYA WANAJAMBO LAO ITALIA

Michezo ya kwanza: Udinese v Como na Inter Milan v Monza, Jumamosi, Agosti 22.

Inter Milan bado ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa Serie A, hasa kwa sababu si timu nyingi zinazoonekana kuwa na uwezo wa kuisumbua.

Napoli, AC Milan, Atalanta na Lazio zote zimeingia msimu huu zikiwa na makocha wapya, huku Juventus na Milan zikiwa kwenye presha baada ya kushindwa kumaliza katika nafasi nne za juu msimu uliopita.

Kukosekana kwao katika Ligi ya Mabingwa kunaweza kuwasaidia katika mbio za ubingwa, ingawa kucheza Europa Ligi siku za Alhamisi ni changamoto mpya kwao.

Mashabiki wa Manchester United pia watakuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa kocha Ruben Amorim kwenye Uwanja wa San Siro.

Napoli, ambayo imeshindwa kutetea mataji yake mawili ya hivi karibuni, sasa matumaini yao yapo kwa kocha Max Allegri kurejesha uwezo wake wa kushinda mataji.

Como ilikuwa moja ya timu zilizovutia zaidi msimu uliopita, lakini swali ni kama kikosi cha Cesc Fabregas kitaweza kurudia mafanikio hayo huku kikicheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa.

Roma ilifanya vizuri na kumaliza nafasi ya tatu msimu uliopita licha ya kuanza vibaya, na imeendelea kumuunga mkono kocha Gian Piero Gasperini katika usajili. Sasa inajiuliza kama inaweza kutwaa Scudetto yake ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 2001.


ULA 03

BUNDESLIGA: NANI ANAWEZA KUMZUIA BAYERN?

Mchezo wa kwanza: Bayern Munich v VfB Stuttgart, Ijumaa, Agosti 28.

Swali la kila msimu nchini Ujerumani bado lipo: Nani anaweza kuizuia Bayern Munich?

Kikosi cha Vincent Kompany kilitwaa mataji mawili ya ndani msimu uliopita huku kikicheza soka la kuvutia.

Harry Kane sasa ana umri wa miaka 33, lakini haonyeshi dalili za kupungua makali. Nahodha huyo wa England amefunga mabao 98 katika mechi 94 za Bundesliga na tayari amevunja rekodi nyingi.

Ingawa kuna maswali kuhusu kipa mwenye umri wa miaka 40 Manuel Neuer pamoja na safu ya ulinzi ya Bayern, nguvu ya ushambuliaji inayoundwa na Kane, Michael Olise na Luis Diaz, pamoja na ujio wa Mmorocco Ismael Saibari, inawapa nafasi kubwa ya kutawala tena.

Borussia Dortmund, RB Leipzig na Bayer Leverkusen zote zina uwezo wa kuwania ubingwa, lakini mara nyingi zimekuwa zikikwama dhidi ya timu za katikati ya msimamo.

Schalke 04, moja ya klabu kongwe nchini humo, inalenga kurejea kuwa timu ya kiwango cha juu baada ya kukaa miaka mitatu nje ya Bundesliga.

Kupanda kwao pia kumerudisha moja ya dabi kali zaidi duniani, Revier Derby dhidi ya Borussia Dortmund.

Elversberg, ambayo ilikuwa ikicheza daraja la nne mwaka 2021/22, imepanda hadi Bundesliga kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Ikiwa na wakazi takribani 13,000, Spiesen-Elversberg itakuwa mji mdogo zaidi kuwahi kuwakilishwa Bundesliga.


ULA 04

LIGUE 1: PSG YAENDELEZA UFALME

Mchezo wa kwanza: Marseille v Strasbourg, Ijumaa, Agosti 21.

Ni vigumu kuona timu nyingine zaidi ya Paris Saint-Germain ikitwaa Ligue 1 kwa mara ya 13 katika misimu 15, hasa baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa mara mbili mfululizo.

Hata hivyo, PSG inaweza kusumbuliwa. Msimu uliopita ilipoteza mechi sita za ligi, idadi iliyozidi kwa jumla mara mbili jumla ya mechi ilizopoteza katika misimu miwili iliyotangulia.

Kocha Luis Enrique ameongeza kiungo mshambuliaji Maghnes Akliouche kutoka Monaco na beki wa kushoto Lucas Digne kutoka Aston Villa.

Hata hivyo, PSG inaweza kuwauza mawinga Bradley Barcola na Ibrahim Mbaye kutokana na kutakiwa na Liverpool.

Monaco na Lille ndizo timu mbili za mwisho kuvunja utawala wa PSG, lakini kwa sasa hazionekani kuwa na nguvu ya kutosha kufanya hivyo tena.

Marseille imekumbwa na changamoto za kifedha ambazo zimeathiri uwezo wake wa kufanya usajili, huku wachezaji wengine muhimu wakitarajiwa kuondoka baada ya Mason Greenwood.

Lens, iliyomaliza ikiwa mpinzani wa karibu zaidi wa PSG msimu uliopita, inaweza kuhitaji muda kuzoea kocha mpya Dino Toppmoller.

Lille, iliyomaliza nafasi ya tatu, iko katika hali kama hiyo baada ya kumteua Davide Ancelotti.

Strasbourg pia imekuwa ikipiga hatua katika miaka ya hivi karibuni, lakini baada ya kuwapoteza makocha Liam Rosenior na Gary O'Neil waliohamia Ligi Kuu England, sasa inaanza upya chini ya kocha asiye na uzoefu mkubwa, Hugo Oliveira.


MENGINE YA KUFUATILIA ULAYA

Katika miaka ya hivi karibuni, klabu za Uturuki zimekuwa zikisajili majina makubwa, lakini uamuzi wa Mohamed Salah kujiunga na Trabzonspor umekuwa mshangao kwa wengi.

Baada ya kuondoka Liverpool mwishoni mwa mkataba wake, Salah alichagua kujiunga na mabingwa wa Super Lig wa msimu wa 2021/22 badala ya Galatasaray, Fenerbahce au Besiktas.

Ikiwa ataiongoza Trabzonspor kutwaa ubingwa, Salah anaweza kuwa shujaa mkubwa wa klabu hiyo.

Nchini Uholanzi, PSV Eindhoven inalenga kutwaa taji la Eredivisie kwa mara ya nne mfululizo.

Ajax na Feyenoord zitalenga kurejea katika ubora wao baada ya misimu iliyopita kuwa ya kukatisha tamaa. Ajax imemteua Mhispania Michel, huku Feyenoord ikimpa mikoba nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi, Giovanni van Bronckhorst.

Nchini Ureno, Porto inalenga kutetea taji la Primeira Liga kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013, lakini inatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake wa Clasico, Benfica, ambayo sasa inaongozwa na kocha Marco Silva.

Sporting CP nayo inajinga kurejesha taji baada ya kulibeba katika misimu ya 2023/24 na 2024/25.