Osimhen achomoza Spurs, kambi yake ikitafakari ofa
Muktasari:
- Osimhen ambaye aliachana na Napoli msimu uliopita na kutua zake jumla Galatasaray alikocheza kwa mkopo msimu mmoja, amekuwa akiwindwa na timu mbalimbali Ulaya na Saudi Arabia ambako wachezaji wengi wamekuwa wakikimbilia katika miaka ya karibuni.
TOTTENHAM Hotspur imewasilisha ofa ya awali yenye thamani ya Pauni 55 milioni kwa ajili ya usajili wa mshambuliaji wa Galatasaray, Victor Osimhen. Hata hivyo, mabingwa hao wa Uturuki wanataka kiasi kinachokaribia Pauni 65 milioni ili kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria mwenye umri wa miaka 27.
Osimhen ambaye aliachana na Napoli msimu uliopita na kutua zake jumla Galatasaray alikocheza kwa mkopo msimu mmoja, amekuwa akiwindwa na timu mbalimbali Ulaya na Saudi Arabia ambako wachezaji wengi wamekuwa wakikimbilia katika miaka ya karibuni.
Katika msimu uliopita mchezaji huyo alifunga mabao 21 na asisti 11 katika mashindano yote ya ndani na nje ya Uturuki, lakini anadaiwa kwamba tangu alipotua nchini humo hana furaha, hivyo ofa yoyote nono itakayomwezesha kutimka inaweza kupokewa kwa mikono miwili na kambi inayomsimamia.
Tangu kuanza dirisha la usajili msimu ujao, mshambuliaji huyo anadaiwa kupokea ofa zaidi ya tano kutoka katika klabu kubwa tatu za England na moja ya Hispania, lakini uamuzi wa kuhamia umekuwa mgumu kutokana na kiasi cha fedha ambacho kinahitajiwa na Galatasaray ambayo imezipiga chini.
Bruno Guimaraes
Arsenal inatarajiwa kukamilisha usajili wa kiungo wa Newcastle United na Mbarazil, Bruno Guimaraes mwenye umri wa miaka 28 anayetarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya, huku dili hilo likiwa na thamani ya karibu Pauni 80 milioni. Nyota huyo anaachana na Newcastle wakati ambapo ikiwa imeanza kukimbiwa na mastaa wake muhimu huku kocha Eddie Howe akimtika zake.
Pep Chavarria
CHELSEA imewasilisha ofa mpya iliyoboreshwa kwa ajili ya beki wa kushoto wa Rayo Vallecano, Pep Chavarria, baada ya klabu hiyo ya Hispania kukataa ofa ya kwanza ya Pauni 12.8 milioni ikitaka Pauni 21.4 milioni kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28. Chavarria anadaiwa kuwa tayari kutimka kikosini kwake kutokana na ugumu wa kupata namba anaokumbana nao.
Lucas Herrington
HULL City inadaiwa kuwa karibu kumsajili beki wa kimataifa wa Australia mwenye umri wa miaka 18, Lucas Herrington, kutoka Colorado Rapids ya Ligi Kuu Marekani (MLS), kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni 17 milioni. Inaelezwa kwamba Herrington amekubali kuondoka Marekani baada ya kuchoshwa na maisha ya huko.
Jack Grealish
ATLETICO Madrid inafikiria kufanya uhamisho wa winga wa England na Manchester City, Jack Grealish ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo katika kikosi cha Everton. Mchezaji huyo wa England mwenye umri wa miaka 30 pia anawindwa na Everton pamoja na klabu yake ya zamani, Aston Villa.
Lukas Hornicek
KIPA wa Braga, Lukas Hornicek, anadaiwa kukamilisha vipimo vya afya na anatarajiwa kujiunga na Newcastle United baada ya klabu hiyo kulipa mkwanja unaotakiwa kulingana na kipengele cha kuvunja mkataba wake chenye thamani ya Pauni 25.7 milioni. Hornicek ana umri wa miaka 24 na ni mchezaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech.
Gonzalo Garcia
MASTAA wa Real Madrid, mshambuliaji Gonzalo Garcia (22 pichani) na kiungo Cesar Palacios (21), wanadaiwa kuwa wangefanyiwa vipimo vya afya jana na Fulham baada ya klabu hizo mbili kukubaliana kuhusu uhamisho wa kudumu wa nyota hao wa kimataifa wa Hispania. Garcia alikuwa na msimu bora uliopita kutajwa katika kikosi kwa mechi, ingawa ni mara chache aliitumikia Madrid.
Cody Gakpo
TOTTENHAM Hotspur imefanya mazungumzo mazuri na mshambuliaji wa Liverpool na Uholanzi, Cody Gakpo, lakini Liverpool haina mpango wowote wa kumuuza nyota huyo mwenye umri wa miaka 26. Katika dili hilo, Spurs imewasilisha mpango wake wa miaka mitatu mezani kwa Gakpo kwa ajili ya kusoma na kuuelewa kabla hajafanya uamuzi.
Mohamed-Ali Cho
HULL City inadaiwa kuwa karibu kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa Nice, Mohamed-Ali Cho kwa ada ya takribani Pauni 17 milioni ambapo nyota huyo wa kimataifa wa Mfaransa mwenye umri wa miaka 22 atasaini kuitumikia kwa miaka mitano. Hata hivyo, pande mbili zingali zinajadiliana juu ya vipengele vingine muhimu.
Jens Hjerto-Dahl
KIUNGO wa Norway, Jens Hjerto-Dahl mwenye umri wa miaka 20 kutoka Tromso anadaiwa kukubali kutua Hull City ambayo inaonekana kuongoza mbio za kumsajili nyota huyo. Hull City inadaiwa kupigana vikumbo na Rangers pamoja na Cardiff City katika mbio za kuwania saini yake, ingawa hadi jana mambo yalikuwa bado hajakamilika.