Barcelona, Real Madrid wamwindia Haaland
Muktasari:
- Man City inakabiliwa na uwezekano wa kukumbana na adhabu kali, ikiwamo kupokonywa pointi nyingi ambazo zinaweza kuishusha timu hiyo daraja, jambo linaloweza kusababisha nyota wake kuanza kufikiria mustakabali wao.
MADRID, HISPANIA: MATAJIRI wa Hispania, Barcelona na Real Madrid, wameanza kuangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, huku mustakabali wa mabingwa hao wa England ukiwa shakani kutokana na tuhuma za ukiukaji wa kanuni za fedha.
Man City inakabiliwa na uwezekano wa kukumbana na adhabu kali, ikiwamo kupokonywa pointi nyingi ambazo zinaweza kuishusha timu hiyo daraja, jambo linaloweza kusababisha nyota wake kuanza kufikiria mustakabali wao.
Miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuathirika na hali hiyo ni Haaland, ambaye bado ana takribani miaka minane kwenye mkataba wake na miamba hiyo ya Etihad.
Barcelona inatafuta mshambuliaji mpya wa kati kuchukua nafasi ya Robert Lewandowski, huku ikionekana kupunguza kasi ya kumwania mshambuliaji mwingine wa zamani wa City, Julian Alvarez.
Kwa upande wa Real Madrid, viongozi wa klabu hiyo wanatajwa kufuatilia kwa karibu hali ya Haaland, licha ya kuwa tayari wanaye Kylian Mbappe anayeongoza safu yao ya ushambuliaji.
Hata hivyo, Real Madrid imekuwa na utamaduni wa kusajili nyota wakubwa duniani, maarufu kama ‘Galacticos’, huku kukiwa na mijadala kuhusu uwezekano wa kuwapanga Haaland na Mbappe katika kikosi kimoja.
Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa Madrid pia inafuatilia hali za Josko Gvardiol, Ayyoub Bouaddi, Elliot Anderson, Enzo Fernandez na Rayan Cherki.
Pamoja na uwezekano wa City kukumbana na adhabu kali, klabu hiyo bado inaweza kudai ada kubwa za uhamisho kwa nyota wake, kwa kuwa inaelezwa kuwa wachache, kama wapo, wenye vipengele vya mikataba vinavyowaruhusu kuondoka iwapo timu itashushwa daraja.
Kiungo wa zamani wa Barcelona, Gaizka Mendieta, amesema anaamini vigogo hao wawili wa Hispania watakuwa na nia ya kumsajili Haaland.
Mshambuliaji huyo raia wa Norway hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Hispania, ambako pia anamiliki nyumba ya mapumziko.
Akizungumzia mustakabali wa Haaland, Mendieta amesema:“Mustakabali wa Haaland unavutia. Tusubiri kuona mambo yatakavyokuwa Manchester City. Lakini wachezaji kama yeye wanataka kushinda mataji.
“Kwa upande wa mahali ninapoweza kumwona, namfikiria akiwa Real Madrid au Barcelona.
“Hata hivyo, nahisi mtindo wa uchezaji wa Barcelona unaweza kumfaa zaidi, na pengine hata klabu yenyewe pia.”