Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Onyo kwa Trent ujio wa Dumfries Madrid

Muktasari:

  • Hiyo ni kwa mujibu wa aliyekuwa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Jimmy Floyd Hasselbaink, ambaye anaamini kuwa ujio wa Denzel Dumfries kutoka Inter Milan utaongeza ushindani mkubwa katika nafasi ya beki wa kulia.

MADRID, HISPANIA: BAADA ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu England ambao hakuwa mzuri sana kwake, Trent Alexander-Arnold atalazimika kuboresha zaidi kiwango msimu ujao ikiwa anataka kumshawishi kocha mpya, Jose Mourinho kwamba anastahili nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid.

Hiyo ni kwa mujibu wa aliyekuwa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Jimmy Floyd Hasselbaink, ambaye anaamini kuwa ujio wa Denzel Dumfries kutoka Inter Milan utaongeza ushindani mkubwa katika nafasi ya beki wa kulia.

Dumfries anatarajiwa kujiunga na Real Madrid mara baada ya kumaliza fainali za Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi na  inaripotiwa kuwa usajili wake utagharimu takribani Euro 20 milioni sawa na kiwango cha kifungu chake cha kuondoka Inter Milan.

Mholanzi huyo anatajwa kuwa usajili wa pili wa rais wa klabu, Florentino Pérez, baada ya kutangazwa kwa Ibrahima Konate.

Hasselbaink alisisitiza kuwa mtindo wa Mourinho unaweza kumpa Dumfries faida zaidi.

"Chini ya Mourinho, nafasi zake ni kubwa kwa sababu Mourinho hupenda mabeki ambao kipaumbele chao kikuu ni kulinda," alisema.

Kauli hiyo inaashiria kwamba Trent bado anatakiwa kuboresha zaidi uwezo wake wa kujihami ili kuendana na matakwa ya kocha huyo.

Kuhusu uwezekano wa Trent kuondoka Real Madrid kutokana na ushindani huo, Hasselbaink alipinga.

"Hapana, sidhani kama anapaswa kuondoka. Anapaswa kuvumilia na kutoa kila kitu. Kwa England, ni jambo zuri kuona wachezaji wa Kiingereza wakicheza nje ya nchi. Sasa una Harry Kane, Anthony Gordon, Marcus Rashford na Trent. Hilo litaisaidia England."

Aliongeza kuwa, "sote tunajua uwezo wa Trent, lakini nguvu zake kubwa ziko kwenye mchezo wa kushambulia. Hata hivyo, kwa kuwa Mourinho ndiye kocha, nafikiri Dumfries atapata dakika nyingi za kucheza," alisema Hasselbaink na kuongeza kuwa, Mourinho atanufaika kwa kuwa na mabeki wawili wa kulia wenye sifa tofauti.

"Ni faida kubwa kwa Mourinho kuwa na mabeki wawili wa kulia wenye mitindo tofauti. Hilo linampa nafasi ya kutumia mbinu mbalimbali za kiufundi kulingana na mchezo."

Pamoja na hayo, Hasselbaink anaamini Trent bado atapata nafasi nyingi za kucheza.

"Bado naamini Trent atacheza sana. Na ndiyo, kutakuwa na ushindani, jambo ambalo ni la kawaida katika klabu kubwa."