Nyota England ashtakiwa kwa kupiga mtu
Muktasari:
- Toney, mwenye umri wa miaka 30 kutoka Northampton, ameshtakiwa kwa kosa la kumshambulia mtu na kumsababishia majeraha ya mwili katika tukio linalodaiwa kutokea Desemba 6, 2025 kwenye klabu moja ya starehe iliyopo Wardour Street, London na anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Westminster, Septemba 24.
LONDON, ENGLAND: MCHEZAJI wa timu ya taifa ya England na Al-Ahli ya Saudia Arabia, Ivan Toney, amefunguliwa mashtaka ya kushambulia mtu kufuatia tukio lililotokea katika klabu ya starehe eneo la Soho, London, Desemba mwaka jana, polisi wamethibitisha.
Toney, mwenye umri wa miaka 30 kutoka Northampton, ameshtakiwa kwa kosa la kumshambulia mtu na kumsababishia majeraha ya mwili katika tukio linalodaiwa kutokea Desemba 6, 2025 kwenye klabu moja ya starehe iliyopo Wardour Street, London na anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Westminster, Septemba 24.
Msemaji wa Toney amesema: “Ivan anakiri kwamba amefunguliwa mashtaka hayo na, ingawa kwa kawaida ameshtushwa na jambo hilo anatarajia kupewa fursa ya kuthibitisha kutokuwa na hatia mahakamani.”
Gazeti la The Sun liliripoti Desemba 8 kwamba Toney alikamatwa baada ya kudaiwa kumpiga mtu kwa kichwa.
Toney, ambaye aliwahi kucheza Brentford, kwa sasa ni mshambuliaji wa klabu ya Al-Ahli inayoshiriki Ligi Kuu Saudi Arabia.
Mchezaji huyo alirejea kutoka Marekani mwezi uliopita, ambako alikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wa England kilichokuwa katika Kombe la Dunia.