Messi avunja ukimya ishu ya mwanawe Barca
Muktasari:
- Ripoti kutoka Hispania zilidai Thiago, 13, angeondoka katika akademi ya Inter Miami na kujiunga na mfumo maarufu wa vijana wa Barcelona maarafu kama La Masia. Hata hivyo, Messi amezima haraka uvumi huo kwa jibu fupi lakini lenye msimamo.
MIAMI, MAREKANI: MJADALA wowote unaohusu familia ya Lionel Messi na Barcelona huvuta hisia kubwa, na wiki hii macho yalielekezwa kwa mtoto wake mkubwa, Thiago Messi.
Ripoti kutoka Hispania zilidai Thiago, 13, angeondoka katika akademi ya Inter Miami na kujiunga na mfumo maarufu wa vijana wa Barcelona maarafu kama La Masia. Hata hivyo, Messi amezima haraka uvumi huo kwa jibu fupi lakini lenye msimamo.
Alipoulizwa na mwandishi mmoja wa habari kama Thiago alikuwa akitarajiwa kuondoka Inter Miami kwenda Barcelona, Messi alijibu kwa neno moja tu; “hapana.” Jibu hilo lilitosha kuweka wazi msimamo wake.
Licha ya kuongezeka kwa taarifa hizo katika vyombo vya habari vya Hispania, Messi alionyesha Thiago ataendelea na maendeleo yake kusini mwa Florida badala ya kurejea klabu ambayo baba yake alijijengea umaarufu mkubwa duniani.
Uvumi kuhusu Thiago ulipata nguvu kutokana na kufanana kwa safari yake na baba’ke na Messi mwenyewe alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa takribani miaka 13 baada ya kuondoka katika klabu ya Argentina, Newell’s Old Boys.
Alitumia zaidi ya miaka 20 Catalunya, akipitia La Masia kabla ya kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya soka.
Katika kipindi chake cha mafanikio Barcelona, Messi alicheza mechi 778, akafunga mabao 672 na kutoa asisti 269, akisaidia kuifanya klabu hiyo kuwa moja ya timu zilizotawala zaidi katika soka la kisasa.
Safari yake Camp Nou ilifikia mwisho 2021 baada ya matatizo ya kifedha kuilazimisha Barcelona kuachana na nahodha wake huyo maarufu. Messi alijiunga na PSG kabla ya kuhamia Inter Miami 2023, ambako amekuwa sehemu ya mradi mkubwa wa kimataifa wa Ligi Kuu Marekani (MLS).
Kwa jibu la Messi inaonyesha kwamba Inter Miami bado ni sehemu muhimu ya mipango ya familia yake na kwamba, Thiago anatarajiwa kuendelea kukua kisoka ndani ya mfumo wa akademi ya klabu hiyo.
Uwezekano wa Messi mwingine kuibuka kupitia akademi ya Inter Miami bila shaka ni simulizi itakayovutia mashabiki wa MLS.
Kauli hiyo pia imekuja wakati Barcelona ikiwa inakabiliwa na masuala makubwa ya usajili na ripoti kutoka Hispania zinaeleza imekubali kushindwa katika harakati zake za kumsajili mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, baada ya Atletico Madrid kuripotiwa kukataa ofa ya karibu Euro 100 milioni. Na sasa inaelezwa kwamba Barca inaangalia mbadala wakiwamo Victor Osimhen na Dusan Vlahovic ili kurithi mikoba ya Robert Lewandowski aliyeondoka.