Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Onguene aweka rekodi WAFCON

ONGUENE Pict

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37 aliweka rekodi hiyo wakati Cameroon ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo wa Kundi D wa WAFCON 2026 uliochezwa kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.

Nyota wa Cameroon, Gabrielle Aboudi Onguene, ameandika historia katika soka la wanawake barani Afrika baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mara nane.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37 aliweka rekodi hiyo wakati Cameroon ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo wa Kundi D wa WAFCON 2026 uliochezwa kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.

Ingawa aliingia uwanjani dakika ya 87 akitokea benchi, Onguene alionyesha bado ana mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Indomitable Lionesses.

Dakika tatu tu alizocheza alileta mabadiliko kwenye safu ya ushambuliaji akileta presha kwa mabeki wa Mali

Akizungumza kuhusu historia hiyo, Onguene alisema anajivunia kuendelea kuitumikia Cameroon kwa kipindi cha karibu miongo miwili tangu alipoanza kucheza WAFCON mwaka 2008.

ONGU 01

Amesema kuvaa jezi ya taifa imekuwa ndoto yake tangu utotoni na kila nafasi anayopata kuitumikia nchi yake ni jambo analolichukulia kwa heshima kubwa.

“Ni heshima kubwa kwangu kuwa hapa na kuendelea kucheza mchezo ninaoupenda. Kuiwakilisha Cameroon imekuwa ndoto yangu kwa miaka mingi,” amesema Onguene.

Mkongwe huyo alifichua kuwa siri iliyomwezesha kudumu kwenye kiwango kikubwa kwa miaka hiyo ni nidhamu. Alisema amekuwa akizingatia mazoezi, lishe bora, mapumziko ya kutosha na kutunza mwili wake, mambo ambayo anaamini ndiyo msingi wa maisha ya mchezaji wa kulipwa anayetaka kudumu kwa muda mrefu.

"Nidhamu ndiyo imekuwa msingi wa kila kitu ninachofanya. Ninautunza mwili wangu, nakula vizuri na kupata mapumziko ya kutosha. Hayo ni mambo muhimu kwa mchezaji wa kulipwa.”

Onguene, ambaye amezaliwa jijini Douala, alisema anajivunia kuzaliwa katika mji uliowahi kutoa nyota wakubwa wa soka la Cameroon kama Samuel Eto'o, Patrick Mboma, Alex Song, Carlos Kameni na Carlos Baleba.

ONGU 02

Katika maisha ya soka, Onguene ameweka historia kubwa.Aliisaidia Cameroon kutwaa medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Afrika mwaka 2011, akafunga bao pekee kwenye Michezo ya Olimpiki ya Uingereza mwaka 2012, kisha akawa sehemu ya kikosi kilichofuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2015, huku bao lake dhidi ya Uswisi likibaki sehemu ya historia ya soka la Cameroon.

Mwaka 2016, Cameroon ilipoandaa WAFCON, Onguene alikuwa katika kiwango bora, licha ya timu hiyo kupoteza fainali dhidi ya Nigeria, alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano.

Ameendelea kung'ara pia ngazi ya klabu baada ya kutwaa mataji matatu akiwa Louves Minproff kabla ya kuhamia Urusi kuichezea Rossiyanka na baadaye CSKA Moscow.

Mbali na rekodi alizoweka, Onguene amesema anatamani urithi wake uwe chachu kwa kizazi kipya cha wachezaji wa Afrika.

"Ujumbe wangu kwa wasichana ni kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uthabiti. Nidhamu ndiyo ufunguo wa mafanikio, na huwa nawakumbusha wachezaji wenzangu kwamba inaweza kutufikisha mbali.”