Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nachula: Kutoka riadha hadi soka

NACHULA Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo Jumanne ya Julai 28 aliingia kwenye vitabu vya historia katika soka la wanawake baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 25 kwenye mechi ya kwanza ya makundi.

Akiwa na umri wa miaka 40, mshambuliaji wa Zambia, Racheal Nachula ameandika historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga bao katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON).

Nachula, ambaye aliwahi kuwa mbeba bendera wa Zambia katika sherehe za kufunga Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, ameonyesha umri sio kikwazo.

Nyota huyo Jumanne ya Julai 28 aliingia kwenye vitabu vya historia katika soka la wanawake baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 25 kwenye mechi ya kwanza ya makundi.

Bao lake la penalti dhidi ya Misri katika mechi ya kwanza wa Kundi C wa WAFCON 2026 lilimfanya kuwa mfungaji mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo.

NACHU 01

KUTOKA MBIO ZA MITA 400 HADI SOKA

Kabla ya kung'ara kwenye soka, Nachula alikuwa mwanariadha mwenye mafanikio makubwa. Alitwaa medali ya shaba katika mbio za mita 400 kwenye Mashindano ya Afrika mwaka 2008 na kufika hatua ya nusu fainali ya Olimpiki za Beijing mwaka huohuo.

Kutokana na mafanikio hayo, alipewa heshima ya kuibeba bendera ya Zambia kwenye sherehe za kufunga Olimpiki hizo.

Ingawa alionekana kuwa na mustakabali mzuri kwenye riadha, lakini alikuwa na ndoto ya kuwa mchezaji wa soka ambaye awali mama yake alimkataza akihofia soka lingeathiri masomo yake.


KUINGIA KWENYE SOKA

Mwaka 2016, akiwa na umri wa miaka 30, Nachula alifanya uamuzi mkubwa wa kuachana na riadha na kuanza maisha mapya ya soka.

Wakati baadhi ya wanamichezo wakianza kufikiria kustaafu katika umri huo, yeye alibadilisha viatu vya mbio na kuvaa viatu vya soka.

Hatua hiyo ilizaa matunda. Aliisaidia Green Buffaloes kutwaa ubingwa Zambia kabla ya kuhamia Ulaya ambako alichezea Zaragoza CFF ya Hispania na baadaye Hapoel Katamon Jerusalem ya Israel.

Uzoefu huo ulimjengea uwezo mkubwa na kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa timu ya taifa ya wanawake ya Zambia, Copper Queens.

NACHU 03

OLIMPIKI MBILI

Baada ya kuiwakilisha Zambia kwenye riadha mwaka 2008, alirejea kwenye Olimpiki za Tokyo 2020 na Paris 2024 akiwa sehemu ya timu ya taifa ya wanawake ya soka na kuandika historia kama Mzambia wa kwanza kushiriki Olimpiki katika michezo miwili tofauti yaani riadha na soka.

NACHU 02

BADO

Katika WAFCON 2026 nchini Morocco, Nachula anashiriki akiwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye mashindano pamoja na Fatoumata Diarra wa Mali.

Kinachovutia zaidi ni kuna tofauti ya miaka 25 kati yake na mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye mashindano, lakini uwanjani tofauti hiyo haionekani wote wanaonekana kuwa na kiwango sawa.

Kocha wa Zambia, Nora Häuptle alisema Nachula ana uwezo mkubwa na kasi kana kwamba ni mchezaji mwenye miaka 20.

"Kwenye kipimo chetu cha mwisho cha uwezo wa kuvumilia mbio za kasi tofauti, Racheal aliwashinda wachezaji wote. Akiwa na zaidi ya miaka 40, hilo linaonyesha bado ana nguvu za ajabu."

Akiwa amecheza winga wa kulia kusaidia safu ya ushambuliaji iliyokuwa na Barbra Banda na Racheal Kundananji, Nachula alifanya kazi kubwa, akailazimisha safu ya ulinzi ya Misri kufanya kosa lililosababisha penalti ambayo yeye mwenyewe aliifunga kwa utulivu.

Häuptle aliongeza "Utulivu wake kwenye tukio lile unaonyesha uongozi wake. Ni mfano bora kwa wachezaji wetu vijana."