Ghana, Cameroon kuna kibarua leo WAFCON
Muktasari:
- Ghana ilianza mashindano kwa kishindo baada ya kuifunga Cape Verde 2-0, huku Cameroon ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali.
BAADA ya kuanza vizuri kwenye fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake WAFCON 2026 kwa ushindi, Ghana na Cameroon leo zinakutana katika mechi ya kuamua ipi itakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutawala Kundi D.
Ghana ilianza mashindano kwa kishindo baada ya kuifunga Cape Verde 2-0, huku Cameroon ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali.
Matokeo hayo yameziweka timu hizo kileleni mwa kundi zikiwa na pointi tatu kila moja.
Hivyo, pambano la leo si la kutafuta ushindi pekee, bali ni vita ya kuwania nafasi ya juu katika kundi.
Ghana ikiwa itashinda, itafikisha pointi sita na kujisogeza karibu zaidi na robo fainali, wakati Cameroon nayo ikitaka kutumia uzoefu wake wa mashindano makubwa kuendeleza mwanzo wake mzuri.
Kwa timu zote mbili, sare pia inaweza kuwa na thamani, lakini ushindi utaipa moja nafasi nzuri zaidi kabla ya mchezo wa mwisho wa kundi. Ghana imeonyesha utulivu katika kuanza kampeni yake, huku Doris Boaduwaa akiwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango bora katika ushindi wa Cape Verde.
Cameroon kwa upande wake, ilionyesha ari ya upambanaji baada ya kuichapa Mali 2-1, huku Ngah Manga akifunga mabao mawili na kuwa shujaa wa mchezo uliopita.
Mchezo huo unakuja wakati ushindani wa Kundi D ukiwa umeanza kutoa picha ya timu zinazoweza kusonga mbele. Mali na Cape Verde, ambazo zote zilifungwa katika mechi zao za kwanza, zitakutana katika mchezo ambao utakuwa wa muhimu kwao kurejea kwenye mbio za kufuzu. Mali ilifungwa 2-1 na Cameroon, huku Cape Verde ikipoteza 2-0 dhidi ya Ghana.
Mshindi kwenye mchezo huo atatanguliza mguu mmoja kwenye robo fainali, huku sare ikiacha mlango wazi kwa kila timu kuelekea mchezo wa mwisho.