Okocha: Sina shaka na Super Eagles, itafuzu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Nigeria itamenyana na Gabon katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Novemba 13, 2025 katika uwanja wa Hide Moulay Hassan nchini Morocco.
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Austin Jay-Jay Okocha, amesema anaamini Super Eagles ina nafasi kubwa ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Nigeria itamenyana na Gabon katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Novemba 13, 2025 katika uwanja wa Hide Moulay Hassan nchini Morocco.
Mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi kati ya DR Congo na Cameroon ili kuwakilisha Afrika kwenye mchujo wa mabara kwa ajili ya tiketi ya Kombe la Dunia 2026.
Akizungumza katika kipindi cha The Exchange na Femi Soneye, Okocha ameeleza imani yake kwa kusema Super Eagles inayonolewa na kocha kutoka Mali Eric Chelle itafuzu kwa Kombe la Dunia.
“Mradi tu kuna mwanga wa matumaini, bila shaka ninaamini Super Eagles itafuzu Kombe la Dunia 2026, pamoja na maajabu ya soka, lakini sina shaka kwamba timu ya taifa langu itafanya vizuri na kuwa sehemu ya timu zitakazokwenda Marekani, Canada na Mexico mwakani,” amesema Okocha.
“Bado nina imani na timu hii inayonolewa na kocha Eric Chelle, ninasisitiza tena sina shaka kabisa kwa hilo, tuna kikosi kizuri na kocha mwenye weledi wa kutosha, hivyo inawezekana kabisa kufuzu Kombe la Dunia 2026. Tunajiweka kwenye hali hii ya kucheza mechi ya mchujo, na ni sisi pekee tunaweza kujitoa hapa na kusonga mbele,” ameongeza Okocha.
Timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, ilimaliza hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 ikiwa katika nafasi ya pili kwenye Kundi C, ambapo ilikabiliana na timu kama Afrika Kusini, Rwanda, Lesotho, Benin, na Zimbabwe.
Licha ya kuanza kwa kusuasua kwa kupata sare na kupoteza baadhi ya mechi za awali, Nigeria ilijipanga na kurejea kwenye ushindani kupitia matokeo bora katika michezo ya mwisho, jambo lililowawezesha kumaliza nyuma ya kinara wa kundi.
Hata hivyo, nafasi hiyo haikuwapa tiketi ya moja kwa moja ya kufuzu Kombe la Dunia, hivyo wamelazimika kuingia kwenye hatua ya mchujo ya Bara la Afrika, ambapo wanakutana na Gabon kwa ajili ya nafasi ya kucheza mechi ya mchujo ya mabara kwa tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.