Obiero ampa siri Mcarthy Harambee Stars
Muktasari:
- Obiero amesema anajisikia vizuri zaidi katikati ya uwanja, ambako anaweza kuunganisha mchezo, kubeba mpira kuelekea mbele na kushirikiana na wachezaji wenzake, licha ya kuwa hana tatizo la kucheza pembeni.
NAIROBI, KENYA: KIUNGO wa Timu ya Taifa ya Kenya maarufu Harambee Stars, Zech Obiero, amempa ujumbe kocha wa kikosi hicho, Benni McCarthy, akifichua nafasi anayopendelea zaidi kucheza na ambayo anaamini inamuwezesha kutumia vizuri uwezo wake.
Obiero amesema anajisikia vizuri zaidi katikati ya uwanja, ambako anaweza kuunganisha mchezo, kubeba mpira kuelekea mbele na kushirikiana na wachezaji wenzake, licha ya kuwa hana tatizo la kucheza pembeni.
“Napendelea zaidi kucheza katikati. Sina tatizo kucheza pembeni, lakini najisikia vizuri zaidi katikati ambako ninaweza kuunganisha mchezo na wachezaji wengine.
“Si sana kucheza mmoja dhidi ya mmoja, bali napenda kuunganisha mchezo, kutumia pasi za akili na kushirikiana na wachezaji wengine. Ingawa nimewahi pia kucheza pembeni,” amesema Obiero.
Kauli hiyo ni ujumbe muhimu kwa McCarthy, ambaye amekuwa akimpa nafasi kiungo huyo katika mipango yake ya Harambee Stars tangu alipompa nafasi kwenye mchezo wake wa kwanza wa kimataifa dhidi ya Estonia mwezi Machi, 2026.
Katika mchezo huo, Obiero alitoa pasi ya bao lililofungwa na Ryan Ogam katika sare ya 1-1, kabla ya baadaye pia kufunga bao katika ushindi wa Kenya wa mabao 3-0 dhidi ya Grenada.
Obiero, mwenye umri wa miaka 21, kwa sasa anaendelea na maisha mapya ya soka baada ya kukamilisha uhamisho wa mkopo kwenda Gillingham, inayoshiriki League Two England, akitokea Leyton Orient.
Akielezea aina ya soka anayopenda kucheza, Obiero amesema nguvu yake kubwa ni uwezo wa kukimbia, kushinikiza wapinzani na kubeba mpira kwenda mbele.
“Ninakuja na nguvu nyingi. Napenda kukimbia, kushinikiza wapinzani na kuupata tena mpira. Ninapokuwa na mpira, napenda kuelekea mbele na pia napenda kuupokea.
“Naweza kuupokea nyuma na kuukokota au kuupokea juu zaidi, kwangu yote ni sawa,” amesema.
Ameongeza kuwa anataka kutumia uwezo huo kusaidia timu kutengeneza nafasi na kupata mabao.
“Ninapenda kusisimua, kupata mpira, kuonyesha uwezo wangu na kujaribu kufunga mabao au kutoa pasi za mwisho. Kwa kiasi kikubwa mimi ni mchezaji anayependa kubeba mpira na kuwa sehemu ya mchezo,” amesema.
Obiero sasa anatarajiwa kuwa sehemu ya mipango ya Harambee Stars katika maandalizi ya mechi za kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Eritrea na Guinea.