Prime
Takwimu Yanga zaipoteza Simba
WAKATI Yanga na Simba zikiendelea kuchuana katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kushinda mechi zao zote tano zilizocheza hadi sasa na kutofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, lakini mabingwa hao watetezi wamewapiga tena bao wapinzani wao.
Yanga inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2026-2027, ikiwa na pointi 15 ambazo ni sawa na za Simba inayoshika nafasi ya pili baada ya zote kushinda mechi tano, ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa tu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Soka Metrics inayojihusisha na ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za Mpira wa Miguu Tanzania, Yanga ndio timu iliyopiga pasi nyingi sahihi hadi sasa, ikizifunika Simba, Azam FC, Singida Black Stars na Pamba Jiji.
Katika mechi tano zilizochezwa, Yanga imepiga jumla ya pasi 2881 na zilizokamilika kwa maana ya sahihi ni 2239, sawa na asilimia 77.7, ikifuatiwa na Azam FC iliyopiga pasi 2294, huku sahihi zilizokamilika ni 1720, ambazo ni asilimia 75.0.
Simba inashika nafasi ya tatu kwa timu zilizopiga pasi nyingi baada ya kupiga 2227 na zilizokamilika kwa maana ya sahihi ni 1597, sawa na asilimia 71.7, huku kikosi cha Singida Black Stars kikifuatia kwa kushika nafasi ya nne.
Singida inayonolewa na Kocha Mkuu, Mkongomani Papy Kimoto, imepiga jumla ya pasi 2220 na sahihi zikiwa ni 1569, sawa na asilimia 70.7, huku Pamba Jiji ikipiga pasi 1213 na kati ya hizo sahihi ni 836, ambazo zote ni sawa na asilimia 68.9.
Katika timu hizo zote zenye wastani mkubwa wa kupiga pasi nyingi ni moja tu ya Pamba Jiji ambayo haiko kwenye nafasi nne za juu ambayo iko nafasi ya 14, ila Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars zinaendelea kuchuana vikali msimu huu.