Nahodha Kenya bado ana matumaini WAFCON
Muktasari:
- Katika mashindano hayo, Kenya ilianza kampeni zake kwa kupoteza mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika Kundi A.
NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Doreen Nabwire, amewataka mashabiki kuendelea kuwa na subira na kuiunga mkono timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, wakati ikiendelea kupigania nafasi ya kufuzu hatua inayofuata ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco.
Katika mashindano hayo, Kenya ilianza kampeni zake kwa kupoteza mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika Kundi A.
Nabwire ambaye ni Mtaalamu wa maendeleo ya soka la wanawake la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) amesema licha ya mwanzo huo mbaya, Starlets bado ina uwezo wa kurekebisha makosa na kupata matokeo mazuri katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Senegal na Algeria.
“Ninaamini kabisa tuna nafasi nzuri dhidi ya Senegal na Algeria, na bado tunaweza kubadilisha hali ilivyo. Morocco ni timu bora yenye maandalizi ya muda mrefu na yenye malengo makubwa. Ni moja ya timu zilizo juu katika viwango vya soka la wanawake barani Afrika,” amesema Nabwire na kuongeza
“Malengo yao hayaishii Afrika pekee. Wanataka kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake na kujijenga kama moja ya timu bora duniani.
“Kenya haikufuzu mashindano haya kwa bahati mbaya. Wachezaji walijitahidi sana kufikia hatua hii. Ingawa matokeo ya kwanza yalikuwa ya kusikitisha, bado tunapaswa kuelekeza nguvu kwenye mechi mbili zilizobaki. Tukipata ushindi katika zote mbili, bado tuna nafasi ya kusonga mbele,” amesema Nabwire.
Mtaalamu Nabwire amesema ukuaji wa soka la wanawake nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla unaendelea kukua kwa kasi, hivyo timu zinapaswa kuwa na ndoto kubwa zaidi ya kushindania ubingwa wa Afrika pekee.
“Tumefikia hatua ambayo soka la wanawake linakua kwa kasi. Lazima tuwe na ndoto za kufuzu Kombe la Dunia. Lakini mafanikio hayategemei yanayotokea uwanjani pekee. Kushinda mechi ni sehemu moja tu ya mambo mengi yanayohitajika ili kufanikiwa,” alieleza.
Nabwire, ambaye aliweka historia mwaka 2009 kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kucheza soka la kulipwa Ulaya baada ya kujiunga na klabu ya SV Werder ya Ujerumani.