Nwabali: Super Eagles itatwaa ubingwa AFCON 2025
Muktasari:
- Nigeria itakuwa inasaka taji la nne katika mashindano hayo, ambayo huchezwa kila baada ya miaka miwili yatakayofanyika nchini Morocco, kuanzia Desemba 21, 2025 na kumalizika Januari 18, 2026.
Kipa wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, Stanley Nwabali amesisitiza kuwa kikosi chao kina uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Nigeria itakuwa inasaka taji la nne katika mashindano hayo, ambayo huchezwa kila baada ya miaka miwili yatakayofanyika nchini Morocco, kuanzia Desemba 21, 2025 na kumalizika Januari 18, 2026.
Timu hiyo ya Afrika Magharibi, ilikaribia kutwaa taji hilo katika mashindano yaliyopita (AFCON 2023), lakini ikapoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Ivory Coast, kwenye mchezo wa fainali.
Nwabali ana matumaini kwamba safari hii watafanikiwa kubeba kombe, kutokana na kuwa na kikosi imara na chenye ubora, huku akijinasibu kurekebisha kasoro ambazo ziliwafanya washindwe kutwaa ubingwa wa mashindano hayo mbele ya Ivory Coast.
“Kama taifa kubwa, daima tunatarajiwa kushinda, siyo tu kushiriki, nina uhakika tutafanikiwa katika kampeni ya kutwaa ubingwa wa AFCON 2025,” Nwabali ameiambia SuperSport TV.
“Tulicheza fainali mwaka jana, nahisi mwaka huu tutalichukua taji. Ninakiri tulifanya makosa madogo hadi kushindwa kufikia malengo katika mashindano yaliyopita, mara hii tumejifunza mambo mengi na tunarudi tukiwa na morari ya hali ya juu,” amesema Nwabali.
Nigeria imepangwa Kundi C pamoja na Tanzania, Tunisia, na Uganda. Mechi ya kwanza itacheza dhidi ya Tanzania Desemba 23, 2025 kisha itapapatuana na Tunisia Desemba 27, 2025 na mechi ya mwisho ya kundi itakuwa dhidi ya Uganda Desemba 30, 2025.
Bingwa mtetezi Ivory Coast imepangwa Kundi F pamoja na Cameroon, Gabon, na Msumbiji. Mechi ya kwanza itacheza dhidi ya Msumbiji Desemba 24, 2025, kisha itakutana na Cameroon Desemba 28, 2025. Mechi ya mwisho ya kundi itakuwa dhidi ya Gabon Desemba 31, 2025.