Ngoma ngumu! Kocha Alonso akwepa swali la Enzo Fernandez
Muktasari:
- Fernandez alipokea mapokezi yaliyokuwa na mchanganyiko katika mchezo wa mwisho wa kirafiki wa Chelsea uliochezwa Stamford Bridge kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: Kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, amekataa kutoa uhakika kwamba kiungo Enzo Fernandez ataendelea kubaki Stamford Bridge msimu huu wa joto, lakini anaamini mchezaji huyo anaweza kuwanyamazisha mashabiki wanaompigia kelele iwapo hatimaye ataondoka na kujiunga na Manchester City.
Fernandez alipokea mapokezi yaliyokuwa na mchanganyiko katika mchezo wa mwisho wa kirafiki wa Chelsea uliochezwa Stamford Bridge kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu England.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kutoka Argentina aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Reece James dhidi ya Real Sociedad na pia akapewa kitambaa cha unahodha. Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Chelsea walimzomea huku wengine wakimshangilia.
Akizungumza siku moja kabla ya kuanza kwa msimu wa 2026/27, huku Chelsea ikitarajiwa kuanza kampeni yake kwa mchezo wa ugenini dhidi ya Fulham Jumatatu, Alonso amesema hali hiyo si jambo la kushangaza katika soka.
“Si jambo lisilo la kawaida. Linaweza kutokea. Tunamuunga mkono. Tunaye mchezaji mkubwa katika Enzo, mchezaji wa kiwango cha juu na muhimu sana.
“Ninafurahi ninapomwona akifanya mazoezi, unaona kwamba ana mawazo ya ushindani. Tunafanya kazi naye kila siku vizuri sana.”
Alonso pia alitoa dalili kwamba Fernandez ataendelea kuwa makamu wa nahodha chini ya James.
Alipoulizwa kama anaamini mashabiki wa Chelsea wataanza kumuunga mkono kiungo huyo, Alonso amesema ana uhakika hali hiyo itatokea mara baada ya mashindano kuanza.
“Nina uhakika hilo litatokea kwa sababu hii ni hali ya kawaida katika soka. Mara tu tunapoanza mashindano, tunahitaji sapoti.
“Tunahitaji kujitolea kikamilifu kutoka kwa timu nzima na mashabiki wote wanapokuja Stamford Bridge. Tunahitaji kusukuma katika mwelekeo mmoja.”
MAN CITY YAMWANIA
Nia ya Manchester City kumnasa Fernandez haijawa siri katika kipindi hiki cha majira ya joto, ingawa timu hiyo inayofundishwa na Enzo Maresca bado haijawasilisha ofa rasmi kwa ajili ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina.
Chelsea awali ilikuwa ikiweka thamani ya Fernandez kuwa pauni 120 milioni, lakini The Blues wamesema masharti hayo ya mauzo yalimalizika pamoja na muda wa mwisho walioweka kwa klabu kuwasilisha ofa, ambao ulikuwa Ijumaa iliyopita.
Manchester City inaweza kupewa bei kubwa zaidi endapo itaamua kuwasilisha ofa mpya kwa sasa.
Hata hivyo, Alonso alikwepa kujibu moja kwa moja maswali yote yaliyohusu iwapo Fernandez ataendelea kuwa mchezaji wa Chelsea, katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya mchezo dhidi ya Fulham.
Badala yake, kocha huyo amesisitiza zaidi namna ambavyo Fernandez amekuwa akifanya vizuri katika mazoezi.
“Enzo ni mchezaji wa Chelsea,” Alonso amesema alipoulizwa moja kwa moja kama Fernandez bado atakuwa Chelsea baada ya siku ya mwisho ya usajili.
“Ni mchezaji wa kiwango cha juu sana. Amekuwa akifanya mazoezi vizuri sana tangu alipoanza siku 10 zilizopita akiwa na timu, ameungana vizuri sana na wenzake.
“Tunafurahi kuwa naye na anajiandaa kwa Jumatatu.
“Anafanya mazoezi vizuri sana. Namwona akiwa na mtazamo mzuri. Hicho ndicho tunachotaka.
“Yeye ni mchezaji, anafanya mazoezi vizuri, anajiandaa kwa Jumatatu na hilo ndilo jambo langu la msingi kwa sasa.”
ALONSO ABADILI MTAZAMO
Fernandez awali alikuwa akitumika zaidi kama namba 10 Chelsea, lakini Alonso alitoa dalili kwamba anamwona mchezaji huyo akicheza katika nafasi ya chini zaidi uwanjani, badala ya kushindana moja kwa moja na Cole Palmer na Morgan Rogers katika nafasi ya juu.
“Anaweza kufanya yote mawili,” Alonso amesema.
“Nadhani akiwa na mpira, ana uwezo wa kuunganisha pasi fupi lakini pia anaweza kupiga pasi ndefu. Ana uwezo wa kuwaona wachezaji walio karibu na walio mbali zaidi na kutoka hapo anaweza kuendeleza mchezo.
“Lakini pia amecheza vizuri sana kama namba 10.”
Hata hivyo, pamoja na kauli hizo za Alonso, hatma ya Fernandez katika kikosi cha Chelsea bado haijawekwa wazi, huku Manchester City ikiendelea kuhusishwa na uwezekano wa kumnasa kiungo huyo wa Argentina.