Chelsea yapandisha dau la Neto
Muktasari:
- Kwa mujibu wa vyanzo vya Chelsea vilivyonukuliwa na Daily Mail Sport, The Blues hawatafikiria kumuuza Neto, 26, kwa kiasi kisichokaribia Pauni 100 milioni.
LONDON, England: CHELSEA imeweka dau la karibu Pauni 100 milioni kwa winga wake Pedro Neto, huku klabu ya Saudi Arabia, Al Hilal, ikionyesha nia ya kumsajili dirisha hili la usajili.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Chelsea vilivyonukuliwa na Daily Mail Sport, The Blues hawatafikiria kumuuza Neto, 26, kwa kiasi kisichokaribia Pauni 100 milioni.
Neto amekuwa akivutia klabu kadhaa ndani na nje ya Ligi Kuu England, huku Al Hilal ikiwa miongoni mwa zinazohusishwa naye kwa nguvu.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa Chelsea kwa ajili ya huduma za nyota huyo wa kimataifa wa Ureno, ingawa viongozi wa klabu hiyo wanafahamu kuna timu zinamtaka.
WANAPANDA THAMANI
Chelsea inaamini thamani ya winga imepanda kwa kiasi kikubwa katika soko la usajili msimu huu, hasa baada ya kufuatilia ada zilizolipwa kwa wachezaji wa nafasi hiyo.
Miongoni mwa mifano ni Yan Diomande, ambaye alihamia Real Madrid akitokea RB Leipzig kwa dili linaloweza kufikia pauni 120 milioni. Wakati huohuo, Paris Saint-Germain imeweka thamani ya zaidi ya pauni milioni 100 kwa Bradley Barcola, ambaye amekuwa akihusishwa na Liverpool.
Chelsea haijawa ikiweka Neto sokoni kwa ajili ya kuuzwa, huku vyanzo vya klabu vikisisitiza kuwa bado wanamthamini sana.
Thamani hiyo pia inaonekana katika bei waliyoweka, licha ya kwamba walimsajili Neto kutoka Wolves mwaka 2024 kwa pauni 54 milioni.
AL HILAL YAONGEZA PRESHA
Neto alianza katika mechi ya kirafiki wa Chelsea dhidi ya Real Sociedad Jumamosi iliyopita na kocha Xabi Alonso alimtumia kama beki wa pembeni upande wa kulia.
Mchezaji huyo alifanya vizuri kabla ya kutolewa dakika ya 76 na nafasi yake kuchukuliwa na Estevao.
Baada ya mechi hiyo, tetesi za kuhamia Al Hilal zimeongezeka, huku ripoti zikidai tayari kumekuwa na makubaliano ya siri kuhusu maslahi binafsi kati ya Neto na klabu hiyo ya Saudi Arabia. Hata hivyo, wawakilishi wake hawajajibu madai hayo walipotafutwa kwa maelezo.
Chelsea ikiamua kumuuza Neto, italazimika kutafuta mbadala wake kabla dirisha la usajili halijafungwa, huku muda uliobaki ukiwa mfupi.
The Blues wamekuwa wakijikita zaidi katika kuwaondoa baadhi ya wachezaji baada ya kufanya usajili kadhaa msimu huu, akiwamo Morgan Rogers, Maxence Lacroix, Pep Chavarria, Marco Palestra, Jordan Henderson na Danny Welbeck.
Chelsea pia inadaiwa kuweka thamani ya Pauni 50 milioni kwa Liam Delap iwapo ataondoka kwa uhamisho wa moja kwa moja. Delap alijiunga na Chelsea akitokea Ipswich baada ya klabu hiyo kulipa kifungu chake cha kuvunja mkataba cha Pauni 30 milioni mwaka uliopita.
Delap bado ana timu zinazomtaka, ingawa haijafahamika kama zitakuwa tayari kufikia bei hiyo ya Chelsea.
Mbali na hilo, Tosin Adarabioyo anawindwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu England pamoja na Benfica ya Ureno, inayofundishwa na Marco Silva. Hata hivyo, Chelsea haijaweka wazi bei wanayotaka kwa beki huyo.