Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atatoboa! Pedro apewa jezi namba 9

PEDRO Pict

Muktasari:

  • Mshambuliaji Delap alijiunga na Chelsea akitokea Ipswich kwa ada ya pauni30 milioni msimu uliopita, lakini alishindwa kuendana na matarajio baada ya kufunga mabao matatu pekee kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la Klabu.

LONDON, ENGLAND: CHELSEA imetangaza namba za jezi ambazo wachezaji wake watatumia msimu huu, huku mshambuliaji Liam Delap akipokonywa jezi namba tisa na kupewa Joao Pedro.

Mshambuliaji Delap alijiunga na Chelsea akitokea Ipswich kwa ada ya pauni30 milioni msimu uliopita, lakini alishindwa kuendana na matarajio baada ya kufunga mabao matatu pekee kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la Klabu.

Kwa jumla, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alifunga mabao matatu katika mechi 47 alizoichezea Chelsea kwenye mashindano yote, kiwango kilichoacha maswali mengi baada ya msimu ambao klabu hiyo pia ilipitia kipindi kigumu chini ya makocha Enzo Maresca na Liam Rosenior.

Tofauti na Delap, Joao Pedro alifanya vizuri zaidi baada ya kujiunga na Chelsea kwa ada iliyoweza kufikia pauni60 milioni akitokea Brighton.

Mshambuliaji huyo Mbrazil alifunga mabao 23 katika mechi 53 za mashindano yote, akawa mmoja wa wachezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea.

PEDR 01

Kutokana na kiwango hicho, Pedro mwenye umri wa miaka 24 amezawadiwa jezi namba tisa msimu huu, huku namba 20 aliyokuwa akiivaa ikiwa bado haijapewa mchezaji mwingine.

Kwa upande wake, Delap amepokea jezi namba 12, ambayo msimu uliopita ilikuwa ikivaliwa na kipa Filip Jorgensen.

Uamuzi huo umeongeza tena mjadala kuhusu kile kinachoitwa “laana ya jezi namba tisa” Chelsea, ambayo kwa miaka mingi imeonekana kuwabebesha mzigo mkubwa washambuliaji waliovaa namba hiyo.

Katika takribani miaka 23 iliyopita, Chelsea imetumia karibu nusu bilioni ya pauni katika kusajili washambuliaji ikiwa na lengo la kupata mrithi wa Jimmy Floyd Hasselbaink, lakini wengi walishindwa kufikia matarajio.

Wachezaji kama Hernan Crespo, Fernando Torres, Radamel Falcao, Gonzalo Higuain, Romelu Lukaku na Pierre-Emerick Aubameyang wote walipitia vipindi vigumu wakiwa wamevaa jezi hiyo.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwa Pedro kuona kama ataweza kuvunja mkosi huo na kuifanya namba tisa kuwa alama ya mafanikio Stamford Bridge.

PEDR 02

Chelsea itaanza msimu wake wa 2026/27 kwa kucheza ugenini dhidi ya Fulham, katika mchezo ambao utakuwa wa kwanza wa ushindani kwa kocha Xabi Alonso akiwa kwenye benchi la timu hiyo.

Historia ya jezi hiyo inaonyesha namna ilivyowahi kuwa mzigo kwa baadhi ya washambuliaji wakubwa waliofika Stamford Bridge.

Romelu Lukaku alijiunga na Chelsea mwaka 2021 kwa ada ya rekodi ya pauni97.5 milioni, akiwa na matarajio makubwa ya kuisaidia timu hiyo kupambana na Manchester City katika mbio za ubingwa.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Ubelgiji alikumbwa na changamoto za utimamu wa mwili na kushindwa kuendana na mfumo wa kocha Thomas Tuchel.

Lukaku alifunga mabao 15 katika mechi 44 kabla ya kurejea Inter Milan kwa mkopo.

Naye Chris Sutton naye alifika Chelsea mwaka 1999 akitokea Blackburn kwa ada ya pauni10 milioni, ambayo wakati huo ilikuwa kubwa. Lakini alishindwa kuendana na presha ya bei hiyo, akifunga bao moja tu katika mechi 39 kabla ya kuuzwa Celtic.

Mshambuliaji Mateja Kezman alifika mwaka 2004 akitokea PSV kwa pauni milioni sita, akitarajiwa kuziba pengo la Hasselbaink.

Baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Uholanzi, Kezman alishindwa kuendeleza kiwango hicho England, akifunga mabao manne katika mechi 25 kabla ya kuuzwa Atletico Madrid.

Chelsea iliwahi pia kumpa jezi namba tisa beki wa Uholanzi, Khalid Boulahrouz, baada ya kumsajili kutoka Hamburg mwaka 2006 kwa pauni milioni tisa.

PEDR 03

Aliyepewa jina la utani “The Cannibal”, Boulahrouz alishindwa kupata nafasi ya kudumu mbele ya John Terry na Ricardo Carvalho. Majeruhi nayo yalimkwamisha na kucheza mechi 20 pekee kabla ya kutumwa kwa mkopo Sevilla.

Mshambuliaji Steve Sidwell alipewa namba hiyo msimu wa 2007/08 baada ya kujiunga na Chelsea kwa uhamisho wa bure akitokea Reading.

Hata hivyo, ushindani wa Michael Essien na Frank Lampard ulimfanya Sidwell acheze mechi 25 pekee kabla ya kuuzwa Aston Villa.

Wakati Franco Di Santo alipewa namba tisa msimu uliofuata baada ya kusajiliwa kutoka Audax Italiano ya Chile kwa pauni milioni nne. Alishindwa kuonyesha makali mbele ya lango, akicheza mechi 16 bila kuacha alama kubwa kabla ya kuuzwa Wigan.

Mshambuliaji Fernando Torres ndiye mmoja wa waliovaa namba hiyo kwa muda mrefu zaidi, kuanzia 2011 hadi 2015. Ingawa bao lake dhidi ya Barcelona Nou Camp mwaka 2012 lilisaidia Chelsea kufuzu kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa, kwa ujumla alishindwa kufikia kiwango kilichotarajiwa baada ya kusajiliwa kwa pauni50 milioni.

PADR 04

Torres alifunga mabao 45 katika mechi 172 za Chelsea, tofauti kubwa na kiwango alichoonyesha Liverpool ambako alifunga mabao 81 katika mechi 142.

Naye Radamel Falcao alifika kwa mkopo mwaka 2015 baada ya kipindi kigumu Manchester United, lakini majeraha na kasi ya Ligi Kuu vilimzuia kuonyesha uwezo wake. Alicheza mechi 12 pekee na kufunga bao moja.

Mhispania Alvaro Morata alisajiliwa kutoka Real Madrid mwaka 2017 kwa pauni60 milioni. Alianza vizuri kwa kufunga mabao 15 katika msimu wake wa kwanza, lakini kiwango chake kilishuka msimu uliofuata, akifunga mabao matano pekee ya Ligi Kuu.

Morata alijaribu hata kubadili namba ya jezi kwenda 29, lakini hakufanikiwa kugeuza mambo na baadaye akarudi La Liga kujiunga na Atletico Madrid mwaka 2019.

Gonzalo Higuain naye alifika Chelsea mwaka 2019 kwa mkopo kutoka Juventus, akiwa mchezaji ambaye kocha Maurizio Sarri aliamini angeweza kumrudisha kwenye kiwango bora baada ya kufanya naye kazi Napoli.

Lakini Higuain aliyefunga mabao 91 katika mechi 146 za Napoli alikuwa mbali na kiwango chake bora England. Alifunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Huddersfield, lakini hakudumu kwenye kiwango hicho.

Baada ya miezi sita, mechi 19 na mabao matano, Higuain alirejea Juventus.

Sasa, Pedro amekabidhiwa jezi hiyo yenye historia nzito. Baada ya kufunga mabao 23 msimu uliopita, mashabiki wa Chelsea wanatumaini Mbrazil huyo atakuwa tofauti na waliomtangulia na hatimaye kuivunja “laana ya namba tisa” Stamford Bridge.