Neymar kuwafuata Messi, Suarez
Muktasari:
- Mkataba wa Neymar na Santos unamalizika Desemba 31, 2026, huku hadi sasa kukiwa hakuna uamuzi rasmi kuhusu kama ataendelea kubaki kwenye klabu hiyo ya Brazil.
MIAMI, MAREKANI: Nyota wa Brazil, Neymar, 34, anaweza kuachana na Santos mwishoni mwa mwaka huu na kuhamia Inter Miami, ambako anaweza kuungana tena na mastaa wenzake wa zamani wa Barcelona, Lionel Messi na Luis Suarez.
Mkataba wa Neymar na Santos unamalizika Desemba 31, 2026, huku hadi sasa kukiwa hakuna uamuzi rasmi kuhusu kama ataendelea kubaki kwenye klabu hiyo ya Brazil.
Mustakabali wa Neymar umeendelea kuibua maswali baada ya tukio lililotokea kufuatia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chapecoense.
Kwa mujibu wa taarifa, Neymar alifika katika kituo cha mazoezi cha Santos, akakaa kwa muda mfupi kabla ya kuondoka bila ruhusa, huku akikosa kushiriki katika mazoezi ya kurejesha nguvu yaliyopangwa kwa wachezaji walioanza mchezo huo.
Tukio hilo lilizua sintofahamu ndani ya klabu, lakini Santos iliamua kutomchukulia hatua za kinidhamu, huku mchezaji huyo akirejea kwenye mazoezi yaliyofuata.
Neymar bado hajafunga mlango wa kuendelea na soka, huku uwezekano wa kubaki Santos, kutafuta klabu nyingine au hata kustaafu ukiwa wazi.
Katika mazingira hayo, Inter Miami imeanza kuonekana kama moja ya vituo vinavyoweza kumvutia, hasa kutokana na uwepo wa Messi na Suarez.
Neymar, Messi na Suarez waliunda moja ya safu hatari zaidi za ushambuliaji duniani walipokuwa Barcelona kati ya mwaka 2014 na 2017.
Katika kipindi hicho, watatu hao walishinda mataji tisa, yakiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji mawili ya La Liga, Copa del Rey mara tatu, Super Cup ya Hispania, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu.
Katika msimu wao wa kwanza pamoja, walikuwa sehemu muhimu ya Barcelona iliyotwaa mataji matatu na kufunga jumla ya mabao 122 katika mashindano yote; Messi akifunga 58, Neymar 39 na Suarez 25.
Sasa, uwezekano wa MSN—Messi, Suarez na Neymar,kuungana tena Miami umeanza kupewa uzito, ingawa bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya Neymar na Inter Miami.
SWALI LA AFYA
Pamoja na mvuto mkubwa wa kibiashara na kimichezo wa kuwakutanisha tena mastaa hao, suala kubwa linaloweza kuamua hatma ya Neymar ni utimamu wake wa mwili.
Akiwa na umri wa miaka 34, sehemu kubwa ya miaka ya hivi karibuni ya Neymar imekuwa ikigubikwa na majeraha na kukosa mwendelezo wa kucheza.
Hata hivyo, kipaji chake bado kinatambulika na kama ataweza kubaki fiti, uwepo wake pamoja na Messi na Suarez unaweza kuwa kivutio kikubwa katika soka la Marekani.
Kwa sasa, Santos bado inamsubiri Neymar afanye uamuzi kuhusu mustakabali wake, huku Inter Miami ikiwa na Messi na Suarez na dirisha la uhamisho likitoa uwezekano wa kutokea kwa muungano mwingine wa kihistoria.