Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vinicius na Arsenal, ngamia katika tundu la sindano

PAZIA Pict


FABRIZIO Romano, mdaku mahiri wa taarifa za ndani za uhamisho wa wachezaji wa soka ambazo zipo nyuma ya pazia majuzi alikuwa katika bifu na mdaku mwingine, Florian Plattenberg. Kila mmoja akijitapa kwamba yupo zaidi katika habari hizo kule majuu.


Wakaibuka watu wengi ambao waliamua ugomvi wao kwa kuwaambia kwamba mtu aliye bora zaidi kwa sasa sio wao. Ni David Ornstein wa mtandao wa Athletic. Labda waliomtaja David walikuwa sahihi zaidi. Na mimi namfuatilia kwa karibu.


Na ghafla David akawa wa kwanza kuivunja hii habari ya kwamba Arsenal walikuwa wanapambana kuipata saini ya staa wa Real Madrid, Vinicius Junior. Ndiyo, Vinicius Junior. Tatizo sio ugumu wa habari yenyewe. Tatizo ni mtoa habari mwenyewe. Anaaminika.

Unaiweka habari ya David katika mizani na kumuamini mtoa habari, lakini unapima ugumu wa uhamisho wenyewe. Vinicius kwenda Arsenal, ambayo pia ni timu yangu, ni moja kati ya uvumi mgumu kuweza kuuamini kuwa unaweza kuwa kweli.

PAZ 01

Kuna sababu nyingi. Nianze na ipi? Kwanza kabisa ili Vinicius ahame Real Madrid kwenda kokote kule inabidi awe mwanasoka ghali zaidi duniani. Na ilitokea kama ajali wakati Paul Pogba alipokuwa mwanasoka ghali zaidi duniani akihama kutokea Juventus kwenda Manchester United mwaka 2016.

Katika hali ya kawaida kwa sasa ni rahisi kuionea ligi kuu ya Italia lakini sioni kama kuna klabu ya England inaweza kumfanya mwanasoka ghali zaidi duniani atokee Hispania na kutua England kama tunavyoshawishiwa katika dili la Vinicius kwenda Arsenal.

Kwa muda mrefu zaidi zama hizi wanasoka walioweka rekodi ni wale wanaotoka England na kwingineko kwenda Hispania. Kabla ya dili la Pogba, mwanasoka ghali wa dunia kutoka England alikuwa Alan Shearer ambaye alihama hapo hapo England kutoka Blackburn Rovers kwenda Newcastle united.

PAZ 02

Baada yah apo tulikutana na rundo la wanasoka ghali ambao walihama ndani ya nchi ya Italia wakati huo mpira wao ukiwa na pesa, kisha baada ya hapo ikahamia Hispania. Ilikwenda hivyo mpaka Pogba alipokwenda United na kisha Neymar akaenda PSG.

Kwa sasa ili mchezaji avunje rekodi ya uhamisho wa dunia nadhani inabidi atoke England aende Hispania. Sioni kama mastaa wakubwa wa Hispania kama akina Kylian Mbappe na Vinicius Junior wakiwa katika nafasi ya England.

Na linapokuja suala la Vinicius unajikumbusha jambo jingine. Ni timu ambayo anataka kwenda Arsenal. Sio kweli. Arsenal haiwezi kuvunja rekodi ya uhamisho wa duniani. Sio moja kati ya sera zao. Hata kuvunja rekodi ya ndani ya England walifanya hivyo kwa mara ya kwanza kwa Declan Rice alipohamia kwao kutoka West Ham. Ilishangaza sana.

PAZ 03

Na kwa namna soko lilivyokaa katika miaka ya karibuni rekodi yenyewe haikudumu muda mrefu ikavunja. Na imevunjwa tena na tena mpaka katika dirisha hili. Akina Elliot Anderson na Morgan Rodgers wameshanunuliwa kwa pesa nyingi dirisha hili. Kumbuka kabla ya hapo rekodi ya Rice ilishavunjwa pia.

Timu ambayo ina mabavu ya pesa ambayo ingeweza kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia ni Manchester United. Wana pesa nyingi. Lakini ni wao ndio ambao walitanuliwa misuli na Real Madrid mwaka 2009 na kulazimika kumuuza Cristiano Ronaldo kwa dau la rekodi. Sir Alex Ferguson alibakia kutoa maneno mengi ya hasira kwa Florentino Perez na genge lake la wahuni.

Timu nyingine ambayo ingekuwa na uwezo mkubwa wa kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia ni Manchester City. Hapa ingeweza kufikirika lakini sio Arsenal. Arsenal wana adabu na pesa yao na ingawa wamekuwa wakijitutumua sana na matanuzi ya manunuzi ya wachezaji sioni kama wanaweza kumchukua mchezaji kama Vinicius Junior.

PAZ 04

Wahuni ambao wanaweza kuvamia jiji la Madrid na kumtwaa Vinicius ni PSG. Hauwezi kuwabishia kwa sababu wana noti za mafuta za Waarabu. Na tayari walishafanya hivyo walipoishangaza dunia kwa kwenda Catalunya kumchukua Neymar.

Hawakuwa na maneno mengi zaidi ya kwenda benki na kuweka kiasi cha pesa ambacho kilikuwepo katika kipengele cha mauzo halali ya Neymar siku akiamua kuondoka. PSG hawashindwi kufanya hivyo kwa Vinicius hata kama dau lake ni kubwa zaidi. Wanaweza kufika hata nusu au robo ya dau na kumchukua kwa kiasi cha Euro 250 milioni.

Pamoja na yote haya mkataba wa Vinicius umebakiza mwaka mmoja tu. Kuna mambo ya kimkataba hayajakaa sawa wakati huu Madrid wakijaribu kukaa naye kitako kumuongezea mkataba mpya. Inadaiwa kwamba Vinicius anamiliki nusu kwa nusu na Madrid suala la haki ya taswira yake katika matangazo ya biashara. Mbappe anamiliki asilimia zake zote.

Bado sioni kwamba Vinicius anaweza kuondoka. Kuna mahala watakaa na kukutana njiani. Jambo jingine ambalo linaweza kuwa na manufaa zaidi kwa PSG kama Vinicius akiamua kuondoka ni ukweli kwamba hawa Watoto wa Amerika Kusini sio mashabiki sana wa kucheza England.

Sio mashabiki sana wa kucheza miji kama London au Manchester. Miji ambayo mvua inanyesha kila kukicha. Wao ni mashabiki wa kucheza zaidi Hispania. Ikishindika basi iwe Paris au Milan.

Akina Ronaldo de Lima, Diego Maradona, Ronaldinho, Rivaldo, Lionel Messi, na wengineo walikwepa kucheza England. Ukiwaambia waende Madrid, Barcelona, Paris na Milan wanawahi kwa haraka.

Kuna mengi nayaona kwamba ni ngumu kwa Vinicius kucheza Arsenal. Ni kama vile Ngamia kupenya katika tundu la sindano. Kama ikitokea basi litakuwa jambo la kustaajabisha. Na zaidi kuna ukweli kwamba Arsenal hainunui mastaa. Huwa inatengeneza mastaa. Sioni kama kuna biashara kama hii inaweza kufanyika.

Labda wakala wa Vinicius anafanya ujanja wa kuiharakisha Madrid kukaa mezani na mteja wake kwa ajili ya dili jipya. Ndiyo, ni mbinu ambayo imekuwa ikitumika mara nyingi na mawakala wa wachezaji wengi wanaosaka mikataba mipya. Wanaongea na waandishi wa habari na kuvujisha kwamba wateja wao wanatakiwa na klabu mbalimbali na kuna ofa zipo mezani.

Kwa hili la Vinicius kwenda Arsenal ningependa kumkubalia David Ornstein, lakini najikuta naishiwa nguvu. Sioni ikitokea.