Neves alimdharau Ronaldo au alilinda mfumo wa Ureno?
Muktasari:
- Wiki hii, kiungo kijana wa Ureno, João Neves, aliingia kwenye mjadala mkubwa baada ya kauli yake alipoulizwa kuhusu nafasi ya Ronaldo ndani ya kikosi hicho.
KATIKA kila mashindano makubwa ambayo timu ya taifa ya Ureno hushiriki, jina la nahodha wake Cristiano Ronaldo, huwa ni sehemu ya mjadala mkubwa duniani kutokana na historia yake kubwa na rekodi alizoziweka katika soka la kimataifa.
Wiki hii, kiungo kijana wa Ureno, João Neves, aliingia kwenye mjadala mkubwa baada ya kauli yake alipoulizwa kuhusu nafasi ya Ronaldo ndani ya kikosi hicho.
Neves alisema kuwa: "Ronaldo hana tofauti na wachezaji wengine. Ni kama mchezaji mwingine yeyote hapa. Wote tunajua hakuna tofauti kubwa; yupo hapa kuisaidia timu kama sisi wengine."
Kauli hiyo ilitolewa kufuatia mchezo wa kuanza kampeni za Ureno katika mashindano ya kimataifa, ambapo walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo, katika mechi ambayo mabeki wa The Leopards walimdhibiti Ronaldo na kumzuia kuonyesha makali yake.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa mitandaoni na miongoni mwa wachambuzi, ikitafsiriwa kwa namna tofauti. Wapo waliodhani Neves amemdharau Ronaldo, huku wengine wakiona alikuwa akisisitiza umuhimu wa mfumo wa timu kuliko mchezaji mmoja.
KWA NINI WENGINE WAMEONA DHARAU?
Kwa mtazamo wa kawaida, ni vigumu kumweka Cristiano Ronaldo katika kundi la wachezaji wa kawaida.
Mshambuliaji huyo amecheza zaidi ya miaka 20 katika kiwango cha juu, amefunga mabao mengi, ameshinda mataji makubwa ya klabu na timu ya taifa, na ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ureno.
Ronaldo ameichezea Ureno mechi 228 na kufunga mabao 143, akiwa mchezaji aliyeweka rekodi ya kipekee katika historia ya taifa hilo.
Yeye ndiye mchezaji pekee aliyefunga katika Euro tano tofauti (2004, 2008, 2012, 2016 na 2020), pamoja na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika Kombe la Dunia tano tofauti (2006, 2010, 2014, 2018 na 2022).
Ndiyo maana kauli ya Neves iliwashangaza wengi, kwani katika historia ya Ureno hakuna mchezaji mwingine aliyefikia rekodi hizo za mechi, mabao na ushawishi mkubwa kama Ronaldo.
Ndani ya mfumo wa timu, Ronaldo anaweza kuonekana kama mchezaji mwingine, lakini katika vitabu vya historia ya Ureno ana hadhi ya kipekee isiyolinganishwa kirahisi.
Ndiyo maana baadhi ya mashabiki waliona kauli ya Neves kama iliyopunguza uzito wa mchango wa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United.
NEVES ALIMAANISHA NINI?
Kwa uchambuzi wa kina wa mazingira ya kauli hiyo, inaonekana Neves alikuwa na ujumbe tofauti.
Soka la kisasa limejengwa zaidi kwenye mifumo ya timu kuliko utegemezi wa mchezaji mmoja.
Mara nyingi makocha husisitiza kuwa mafanikio hayawezi kubebwa na nyota mmoja pekee, hata kama ana kiwango cha juu kiasi gani.
Huenda Neves alilenga kupunguza presha inayowekwa kwa Ronaldo kila Ureno inapocheza.
Kwa miaka mingi, matokeo ya Ureno yamekuwa yakihusishwa moja kwa moja na Ronaldo; timu ikishinda anasifiwa, ikipoteza lawama zinaelekezwa kwake.
Hata hivyo, kikosi cha sasa cha Ureno kina wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa kama Bruno Fernandes, Bernardo Silva, Rafael Leão, Vitinha, Gonçalo Ramos na João Neves mwenyewe.
Kwa mtazamo huo, kauli yake inaweza kufasiriwa kama msisitizo kwamba kila mchezaji ana mchango sawa ndani ya mfumo wa timu.
HII SI MARA YA KWANZA
Hii si mara ya kwanza kwa mjadala kama huu kujitokeza ndani ya kikosi cha Ureno.
Baada ya Ronaldo kufunga hat-trick dhidi ya Hispania kwenye Kombe la Dunia 2018, kocha wa wakati huo Fernando Santos alisisitiza kuwa timu haimtegemei mchezaji mmoja.
"Soka si mchezo wa mtu mmoja. Si kuhusu Cristiano Ronaldo pekee," alisema Santos.
Vilevile, baada ya Euro 2020, Bruno Fernandes alieleza kuwa mafanikio ya timu hayawezi kuhusishwa na mchezaji mmoja, bali ni juhudi za kikosi kizima.
Kauli hizi zote zinaonyesha mtazamo unaoendelea ndani ya Ureno: kujenga timu badala ya kutegemea nyota mmoja.
UKWELI ULIPO
Kauli ya Neves huenda ilikosa maneno ya kidiplomasia ambayo yangepunguza tafsiri tofauti.
Inawezekana angeweza kusema Ronaldo ni mchezaji muhimu lakini mafanikio ya timu yanategemea kikosi kizima. Hata hivyo, kuichukulia kauli hiyo kama dharau ya moja kwa moja kunaweza kuwa si sahihi.
Ukweli unabaki kuwa Ronaldo si mchezaji wa kawaida katika historia ya Ureno, lakini kwa upande mwingine, soka la kisasa linazidi kuelekea kwenye mfumo wa pamoja badala ya utegemezi wa mtu mmoja.
Ndiyo maana kauli ya Neves imeendelea kuibua mjadala mkalikwa wengine ikiwa ni kawaida, na kwa wengine ikiwa ni kauli nzito inayogusa historia ya mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi duniani.