Malaga yafunga penalti goli tupu baada ya Fulham kutoka Uwanjani
Muktasari:
- Malaga ilisawazisha dakika ya mwisho ya muda wa kawaida na kufanya matokeo kuwa 2-2 baada ya beki wa Fulham, Calvin Bassey, kuadhibiwa kwa kuushika mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari.
MALAGA, HISPANIA: MCHEZO wa kirafiki kati ya Malaga na Fulham ulimalizika kwa tukio la kushangaza jana Jumatano, baada ya Malaga kupiga penalti kwenye goli tupu wakati wachezaji wa Fulham wakitoka uwanjani.
Malaga ilisawazisha dakika ya mwisho ya muda wa kawaida na kufanya matokeo kuwa 2-2 baada ya beki wa Fulham, Calvin Bassey, kuadhibiwa kwa kuushika mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari.
Eneko Jauregi alifunga penalti hiyo na kuifanya Malaga isawazishe, lakini tukio hilo lilikuwa mwanzo wa vurugu za aina yake.
Kocha wa zamani wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa, alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonekana akimlalamikia mwamuzi mwishoni mwa mchezo.
Arbeloa kisha alielekea moja kwa moja vyumbani akiwa ameambatana na wachezaji wake, ambao waliamini mchezo ulikuwa umefikia mwisho.
Hata hivyo, Malaga walibaki uwanjani wakisubiri mikwaju ya penalti ili kumpata mshindi wa Costa del Sol Trophy.
Wakati mashabiki wakisubiri mikwaju hiyo, mshambuliaji Jauregi aliweka mpira kwenye alama ya penalti na kupiga shuti lililoingia kwenye lango tupu, kabla ya kusherehekea na wachezaji wenzake mbele ya mashabiki wa Malaga kwenye Uwanja wa La Rosaleda, kusini mwa Hispania.
Fulham ilisisitiza kuwa timu hizo mbili zilikubaliana kabla ya mchezo kwamba endapo wangetoka sare, hakutakuwa na mikwaju ya penalti.
“Kabla ya mchezo, tunaweza kuthibitisha kuwa timu zote mbili zilikubaliana kwamba hakutakuwa na mikwaju ya penalti endapo mchezo ungeisha kwa sare,” Fulham iliandika kupitia X.
Hata hivyo, katika taarifa yake baada ya mchezo, Malaga ilisema: “Ingawa mikwaju ya penalti ilikuwa imepangwa, Fulham iliondoka uwanjani ikidai kwamba mikwaju hiyo haikuwekwa kwenye mkataba.”
Fulham itamaliza maandalizi yake ya msimu kwa kucheza dhidi ya Stuttgart Jumamosi.
Mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England msimu wa 2026/27 utakuwa dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Craven Cottage, Jumatatu, Agosti 24.