Mziki wa Chelsea utakuwa moto balaa
Muktasari:
- Ripoti zinafichua kwamba Chelsea ipo kwenye mazungumzo ya kumsajili Sancho kwa mkopo wa msimu mmoja huku kukiwa na kipengele cha kumchukua jumla kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi 2025.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA itakuwa na kikosi matata kwelikweli endapo kama itafanikiwa kukabilisha dili za kuwanasa Victor Osimhen na Jadon Sancho.
Ripoti zinafichua kwamba Chelsea ipo kwenye mazungumzo ya kumsajili Sancho kwa mkopo wa msimu mmoja huku kukiwa na kipengele cha kumchukua jumla kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi 2025.
Sancho anajitafuta kurudi kwenye ubora wake baada ya kushindwa kutoa ushawishi kwenye kikosi cha Manchester United.
Na atakwenda moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza endapo kama atatua Stamford Bridge.
Nafasi ambayo inadaiwa kuwa bora zaidi kwa Sancho ni kwenye wingi ya kushoto. Hilo ni eneo ambalo Chelsea imeshindwa kulifanyia kazi vizuri kutokana na mawinga Raheem Sterling na Mykhailo Mudryk kuwa na viwango vya kupanda na kushuka kama homa za vipindi.
Hivyo, Sancho anaweza kwenda kuunda safu matata kabisa ya fowadi ya wakali wanne sambamba na Osimhen.
Chelsea inaamini itakamilisha dili la kumsajili straika huyo wa Napoli kabla ya dirisha hili kufungwa. Lakini, kufanya hivyo watalazimika kuvunja benchi, la kama watawafanya Napoli kukubali kumchukua straika Romelu Lukaku kwenye dili la kubadilishana wachezaji.
Kwenye eneo mengine, Christopher Nkunku na Cole Palmer ni wakali wengine watakaokuwa na uhakika wa kuanza kwenye kikosi cha Enzo Maresca, hiyo ina maana Pedro Neto na Noni Madueke wataanzia benchini sambamba na Nicolas Jackson.
Kwenye safu ya kiungo kutakuwa na Enzo Fernandez na Moises Caicedo huku Romeo Lavia na Kiernan Dewsbury-Hall watasubiri kwenye benchi, wakati kwenye safu ya mabeki, kutakuwa na Reece James na Marc Cucurella watakaopata nafasi mbele ya Malo Gusto, Renato Veiga na Ben Chilwell huku Axel Disasi, Tosin Adarabioyo na Benoit Badisahile wataanzia benchi mbele ya Wesley Fofana na Levi Colwill.
Golini, Filip Jorgensen anaweza kuwa chaguo la kwanza mbele ya Robert Sanchez, ambaye anatazamwa kama chaguo la pili kwenye eneo hilo.