Prime
Doumbia aibua jipya Simba, viongozi watajwa!
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Ibrahim Doumbia, ameanza kukutana na presha mapema baada ya kushindwa kuonyesha makali katika michezo minne ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara, huku wadau wa soka wakihoji kama usajili ulifanywa kwa kuangalia takwimu pekee au uwezo halisi.
Aliyekuwa kocha na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee kufunga mabao matatu (hat-trick) katika mchezo mmoja wa Dabi ya Kariakoo amesema kiwango cha Doumbia hadi sasa hakijampa sababu ya kuona kuwa mshambuliaji huyo anaweza kuonyesha thamani yake.
Kibadeni ambaye aliweka rekodi hiyo Julai 19, 1977, kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam ambapo Simba iliibuka na ushindi mnono wa kihistoria wa 6-0 dhidi ya Yanga, amesema tatizo kubwa la Doumbia ni namna anavyocheza na kushindwa kuonyesha ubora unaoweza kuleta tofauti.
“Nimecheza kwa kiwango kikubwa cha ushindani na nimefundisha pia, kwa hiyo nina uelewa mkubwa wa mpira. Inaweza isiwe mimi, lakini ni muhimu katika eneo nyeti kama hilo kuwa na watu wenye uelewa mkubwa wa mpira. Tusifike mahali tukasajili kwa kuangalia takwimu tu za mchezaji, ni vizuri pia kuangalia staili yake ya uchezaji,” amesema Kibadeni.
Doumbia ambaye hadi sasa ametumika katika mechi tano, moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, huku nne zikiwa za Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, Pamba Jiji, Singida Black Stars na Coastal Union, alitua Simba akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Mali 2025-2026 baada ya kufunga mabao 17 akiwa na AS Korofina.
Kibadeni amesema, pia kushindwa kwa washambuliaji wazawa kuonyesha makali kumewafanya viongozi wa klabu kubwa kuendelea kutafuta masuluhisho nje ya Tanzania, akisema baadhi ya wageni wanaosajiliwa wanashindwa kuonyesha thamani zao Ligi Kuu Bara.
“Lakini pia naamini haya yamechangiwa na wachezaji wazawa kushindwa kuonyesha. Kama kungekuwa na washambuliaji wengi wazawa wenye uwezo wa kutisha, pengine viongozi wasingekuwa wanahangaika sana na wachezaji wa kigeni. Ninathamini mchango wa baadhi ya wachezaji wa kigeni, lakini wapo ambao hakuna kitu wanafanya. Tazama leo Simba ndiyo inahangaika hata kufunga bao moja dhidi ya Coastal,”amesema.
Kwa upande wake mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Jamil Mchaulu ‘Baloteli’ amesema Watanzania wanapaswa kuacha kupima ubora wa washambuliaji kwa idadi ya mabao pekee, akisema aina ya mpira anaocheza mchezaji ndiyo inayopaswa kuwa sehemu kubwa ya tathmini kabla ya mabao.
“Wapo washambuliaji wengi ambao walikuwa wanafanya vizuri huko lakini walipofika hapa walishindwa, jambo muhimu ni kuwa na tathimini kubwa ambayo hata kama mchezaji atafeli basi itakuwa ni shida za mchezaji mwenyewe na sio hivi,” amesema.
Hata hivyo, wakati Kibadeni na Mchaulu wakisisitiza umuhimu wa kuangalia ubora halisi wa mshambuliaji, straika mwingine wa zamani aliyewahi kuzichezea Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Botswana Defence Force XI na Taifa Stars, Rashid Mandawa, amekuwa na mtazamo wa kumpa Doumbia muda zaidi.
Amesema mshambuliaji anaweza kupitia kipindi kigumu mwanzoni baada ya kuhamia timu mpya kutokana na tofauti za mfumo, mazingira na namna anavyotumiwa, hivyo michezo minne haitoshi kutoa hukumu ya mwisho kuhusu uwezo wa Doumbia.
“Kuna wachezaji ambao wamekuwa wakiendana na mazingira mapya taratibu sio wote ambao wanaweza kujiunga na timu mpya kisha wakaanza kuonyesha makali yao hapohapo hivyo tuendelee kumpa muda,” amesema Mandawa.
Mandawa anaamini mshambuliaji huyo anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Simba endapo atapata muda wa kuzoea mazingira na mfumo wa timu huku akisisitiza kuwa presha ya sasa haipaswi kumfanya mchezaji ahukumiwe mapema.