Kila timu hesabu ni fainali CECAFA
Muktasari:
- Mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Kawempe Muslim Ladies FC ya Uganda dhidi ya Commercial Bank of Ethiopia (CBE), timu hizo zinatarajiwa kuingia uwanjani saa 7:00 mchana.
LEO, Jumamosi Agosti 29, 2026, macho ya mashabiki wa soka la wanawake yanaelekezwa Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda, ambako michezo miwili ya nusu fainali ya mashindano ya CECAFA itachezwa kusaka timu zitakazocheza fainali.
Mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Kawempe Muslim Ladies FC ya Uganda dhidi ya Commercial Bank of Ethiopia (CBE), timu hizo zinatarajiwa kuingia uwanjani saa 7:00 mchana.
Kawempe ilikuwa Kundi B, ambako ilianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya CBE. Agnes Nabukenya ndiye aliyefunga bao la ushindi kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 11.
Baadaye Kawempe ilimalizia kazi kwa kuichapa FC Ujeco ya Djibouti mabao 8-0, ushindi uliowapeleka hatua ya nusu fainali. Kocha Ayub Khalifa Kiyingi amesema timu yake ilifurahia kufikisha ushindi huo na kufunga mabao tisa bila kuruhusu bao katika michezo yao miwili.
CBE ilianza kwa kishindo, ikiifunga FC Ujeco mabao 11-0. Hata hivyo, ilikwama mbele ya Kawempe na kupoteza 1-0. Pamoja na kipigo hicho, CBE ilifanikiwa kufuzu kama timu ya pili bora kutoka makundi yote kutokana na tofauti nzuri ya mabao.
Hivyo, mchezo wa leo utakuwa nafasi ya CBE kulipa kisasi cha kipigo cha hatua ya makundi, wakati Kawempe itataka kuthibitisha kuwa ushindi wao wa kwanza haukuwa wa bahati. Hapa kila timu inahitaji dakika 90 za umakini ili kufika fainali.
Mchezo wa pili utakuwa kati ya Yei Joint Stars ya Sudan Kusini na Kenya Police Bullets ya Kenya, ukipigwa saa 10:00 jioni katika uwanja huo huo, Yei inaingia ikiwa moja ya timu zilizofanya vizuri zaidi kwenye hatua ya makundi.
Yei iliongoza Kundi A kwa pointi saba baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare moja, Ushindi wake muhimu ulikuwa wa 1-0 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar, kabla ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji Rayon Sports na kufuzu kwa mara ya kwanza kwa nusu fainali.
Kwa Yei, kufika hapa tayari ni historia, timu hiyo ilikuwa ikishiriki mashindano haya kwa mara ya sita, lakini haijawahi kufika hatua hii na imebaki hatua moja tu kuingia kwenye fainali.
Kenya Police Bullets nayo imeonyesha ubora wake, ilianza kwa kuifunga Simba Queens ya Tanzania 2-1, kisha ikamalizia kwa kuifunga FC Ujeco 3-1.
Kwa hiyo, Police Bullets inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na uzoefu wa hatua za juu, baada ya kuwa mshindi wa pili mwaka 2024.
Na mashindano haya ya 2026, hakuna hatua tofauti ya robo fainali kama ilivyo kwenye mashindano mengine. Baada ya hatua ya makundi, timu zilizofuzu ziliingia moja kwa moja kwenye nusu fainali.
Bingwa wa mashindano hayo ndiye atakayepata tiketi ya kuiwakilisha CECAFA kwenye CAF Women’s Champions League 2026, hivyo Kigali leo itakuwa na vita ya kweli ya kutafuta fainali.