MZEE WA UPUPU: Kusuasua kwa Chelsea, nini hakiendi sawa darajani?

MABINGWA wa klabu bingwa ya dunia, Chelsea FC, wanapitia moja ya nyakati ngumu zaidi ndani ya karne ya 21. Walimaliza msimu uliopita bila taji lolote. Klabu bingwa ya dunia ilikuwa kwa ajili ya msimu wa nyuma yake japo mashindano yalifanyika Februari 2022.
Hata hivyo, msimu haukuwa mbaya kama ulivyo msimu huu. Wanasamawati hao walimaliza Ligi Kuu ya England katika nafasi ya tatu kwenye ligi na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pia walifika fainali mbili na kupoteza zote kwa mikwaju ya penalti, Kombe la Carabao na Kombe la FA...siyo mbaya sana!
Lakini msimu huu wa 2022/23 umekuwa wa hovyo kuliko hovyo yenyewe. Mabosi walielekeza nguvu kwenye kikosi ili kuongeza ubora na kununua wachezaji kama Wesley Fofana, Marc Cucurella, Raheem Sterling na wengine wengi na kuwapeleka Darajani kulinda heshima.
Japo kufukuzwa kazi kwa kocha Mjerumani Thomas Tuchel kulikuja kama jambo la kushtua, lakini kazi nzuri ya Graham Potter klabuni Brighton iliwafanya wengi waamini kwamba ametoka NTU na amekuja NTU.
Hata hivyo, mambo hayajawa kama yalivyotarajiwa. Alama 29 kwenye michezo 20 zimeifanya Chelsea kuanguka nafasi ya 10 kwenye msimamo, alama 10 nyuma ya nafasi nne za juu na alama 21 nyuma ya vinara Arsenal...balaa!
Tayari msimu wao wa Kombe la FA umeisha, tena kwa aibu kubwa baada ya kichapo cha 4-0 kutoka Manchester City dimbani Etihad. Maumivu ni mengi kwa watukutu wa Darajani na kila mmoja anajiuliza nini kimebadilika kwa The Blues.
Yafuatayo ni mambo matano ambayo safu hii inayaona kama sababu za kuyumba kwa mabingwa hao mara mbili wa Ulaya.
1. Kuondoka mihimili ya timu, maingizo mapya
Antonio Rudiger, Andreas Christensen, Timo Werner, Marcos Alonso na wengine wengi wameondoka Chelsea. Kuwapoteza nyota wote hao kwa pamoja siyo kitu rahisi cha kupita hivihivi bila kuitingisha klabu yoyote.
Klabu ilijitahidi kutafuta watu wa kuziba nafasi kama Raheem Sterling, ambaye kwa sasa ndiye mfungaji bora wa Chelsea kwenye Ligi Kuu. Pia ujio wa chipukizi wengine kama Omari Hutchinson ulileta matumaini.
Lakini hata hivyo kulikuwa na sajili zenye kutoa shaka. Klabu ilichagua kuleta watu wenye uzoefu kama Khalidou Koulibaly na kumwaga pesa ndefu kwa Cucurella. Pia usajili wa Pierre-Emerick Aubameyang, mchezaji ambaye ameshapita umri wa ubora wake, na mwisho mwisho ni Denis Zakaria.
Wachezaji hawa wote hawajaonyesha thamani yao Darajani licha ya matarajio makubwa katika uwekezaji wa klabu kwao.
Cucurella na Koulibaly wanahangaika kuzomea namna ya uchezaji ya Chelsea, mabao Aubameyang yamekauka huku Fofana aKiendelea kupambana na majeraha. Sajili hizi zote ni mfano wa zile za hamaki ambazo Chelsea ilizifanya kuelekea kuanza kwa msimu huu.
Kutokana na kizunguzungu cha kuwapoteza nyota wake, Chelsea imeingia sokoni kwa hamaki na kuzoa yeyote aliyekatiza mbele yao.
2. uuzwaji Chelsea uligubikwa na sintofahamu
Mwishoni mwa msimu uliopita akaunti zote za klabu zilipigwa tanji, moja kwa moja hali hiyo ikaathiri utulivu wa akili wa wachezaji na watu wote wa benchi la ufundi.
Hatimaye klabu ikauzwa kwa taikuni wa Kimarekani,Todd Bohely, lakini mambo bado hayakutengamaa.
Kulikuwa na ripoti kadhaa za mabishano na kutokubaliana kuhusu usajili kati ya bosi mpya na kocha Thomas Tuchel, mfano mzuri ni usajili Cristiano Ronaldo.
Bosi alitaka kumsajili nyota huyo aliyekosa amani Old Trafford, lakini Tuchel akakataa...hali ya hewa ikaanza kuchafuka. Sintofahamu na kupishana maono kati ya kocha na bosi mpya vikafika mbali na kuathiri kibarua cha Mjerumani Tuchel ambaye alionekana kuwa kocha sahihi kwa Chelsea.
3. Pupa mabadiliko bosi mpya
Baada ya timu kuangukia kwa Boehly, hapohapo akaanza mchakato mrefu wa kufukuza chizi na makopo yake.
Alimtoa Marina Granovskaia, mtendaji aliyeijulia Chelsea kwa miaka mingi. Akamtoa Mwenyekiti Bruce Buck aliyedumu katika kituo hicho kwa miaka mingi. Akamtoa Guy Laurence, mtendaji mkuu wa klabu hiyo. Akamtoa Petr Cech, mshauri wa ufundi na ufanisi. Na mwisho kufukuzwa kwa kocha Thomas Tuchel.
Hawa walikuwa watu muhimu katika kila kitu cha Chelsea kuanzia usajili hadi matokeo. Timu mpya ya uongozi aliyoileta ipo katika kipindi cha mpito kujuana yenyewe na kujua namna gani mambo yanaendeshwa ndani ya klabu.
4. Kukosa misingi ya kiufundi ya muda mrefu
Licha ya mafanikio makubwa ya Chelsea chini ya Roman Abramovich, lakini klabu hiyo iliishi maisha ya dharura kwa kutegemea mipango ya muda mfupi. Ndani ya miaka 20 ya Abramovich, Chelsea imefukuza makocha 17 kutokana na sababu mbalimbali.
Hii ina maana kwamba makocha wote walikaa kwa muda mfupi klabuni hapo, hivyo kukosa muda wa kujenga misingi sahihi na badala yake kujikita katika kutafuta ushindi kwenye mchezo ujao tu.
5. MAJERAHA
Kocha wa zamani wa Brighton, Potter alipewa kuiongoza klabu hiyo baada ya kuondoka Tuchel. Hata hivyo, msimu wa kwanza umeandamwa na majeraha ya wachezaji muhimu. Potter amekuwa hana kikosi bora kwa kuwakosa wachezaji muhimu kama Ben Chilwell, Reece Hames, Wesley Fofana, NíGolo Kante, na hata Ruben Loftus-Cheek kutokana na majeraha. Katika orodha hiyo pia wapo Edouard Mendy, Denis Zakaria, Pulisic na Broja
Chelsea ina kazi ya kufanya kujikwamua kutoka lindi hili la matatizo, la sivyo itajikuta ikipitia kipindi kirefu cha machungu kama Liverpool au Man United na Arsenal.