Kisa Enzo: Chelsea yaitega Man City
Muktasari:
- Fernandez ni nahodha msaidizi wa Chelsea, amekuwa akishinikiza kuondoka klabuni hapo tangu Machi, huku akihusishwa pia na mpango wa kujiunga na Real Madrid ya Hispania.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imeipa Manchester City hadi saa 11:00 kesho Ijumaa jioni kukamilisha dili la kumsajili kiungo Enzo Fernandez kwa ada ya pauni 120 milioni.
Fernandez ni nahodha msaidizi wa Chelsea, amekuwa akishinikiza kuondoka klabuni hapo tangu Machi, huku akihusishwa pia na mpango wa kujiunga na Real Madrid ya Hispania.
Kocha wa zamani wa Chelsea, Enzo Maresca, ambaye sasa ameichukua Manchester City baada ya kuchukua nafasi ya Pep Guardiola, anatamani kukutana tena na Fernandez katika kikosi chake.
Manchester City inamuhitaji Fernandez kama sehemu ya mpango wa kuziba pengo la kiungo Rodri endapo Mhispania huyo ataondoka Etihad.
Rodri anatajwa kuwa na shauku ya kujiunga na Barcelona, lakini City imekataa ofa ya pauni 55 milioni kutoka kwa miamba hiyo ya Hispania.
City inamthamini Rodri kwa pauni 70 milioni, ingawa kuna taarifa kutoka Hispania kwamba inaweza kushawishika kufanya biashara ikiwa ofa itazidi pauni60 milioni, kutokana na mkataba wa mchezaji huyo kubakiza chini ya mwaka mmoja.
Muda wa mwisho uliowekwa na Chelsea kwa Fernandez inaweza kuipa Barcelona nguvu zaidi kwenye mazungumzo na City, hasa kutokana na hofu kwamba Maresca anaweza kubaki bila kiungo muhimu iwapo Rodri ataondoka.
Fernandez (25), aliikosoa Chelsea kwa uamuzi wa kumtimua Maresca katika mahojiano aliyofanya akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa mwezi Machi.
Katika kipindi hicho, wakala wake Javier Pastore amesema hadharani kuwa mteja wake analipwa chini ya thamani yake na angependa kuondoka Chelsea, kufuatia msimu mgumu ambao klabu hiyo ilimaliza nafasi ya 10 kwenye Ligi Kuu England na kukosa taji baada ya kufungwa na Manchester City katika fainali ya FA Cup.
Hata hivyo, Chelsea haijawa tayari kushusha bei yake ya pauni120 milioni na tayari imeiambia City kuwa iwapo haitatimiza kiasi hicho kabla ya saa 11:00 jioni Ijumaa, Fernandez atasalia Stamford Bridge.
Endapo dili hilo litashindikana, kiungo wa City, Elliot Anderson, anaamini ana baadhi ya sifa zinazofanana na Rodri na anaweza kusaidia kuziba pengo lake kwenye kiungo.
Anderson, mwenye umri wa miaka 23, amesema: “Ndiyo, ninaweza kufanana naye kwa baadhi ya mambo. Nina uwezo wa kufanya majukumu mbalimbali ndani ya kiungo.
“Naweza kucheza popote na kutengeneza nafasi, kuanzisha mashambulizi mbele au kucheza katika nafasi nyingine.”
Kocha mpya wa Chelsea, Xabi Alonso, tayari amesema angependa Fernandez abaki Stamford Bridge.
Fernandez alifunga mabao 15 na kutoa asisti saba katika mechi 54 alizoichezea Chelsea msimu uliopita.
Baadaye aliisaidia Argentina kufika fainali ya Kombe la Dunia, ambapo alitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo ambao Argentina ilifungwa 1-0 na Hispania.
Fernandez amerejea mazoezini na Chelsea wiki hii kwa mara ya kwanza chini ya kocha Alonso, huku mustakabali wake ukibaki kusubiriwa kwa hamu hadi muda wa mwisho wa Ijumaa.
Hata hivyo, Chelsea imeanza kufuatilia uwezekano wa kumsajili kiungo mwingine kama mbadala iwapo Fernandez ataondoka.
Bournemouth ilikataa ofa ya pauni milioni 64 ya kumsajili Alex Scott mapema katika dirisha hili la usajili. Chelsea haijarudi na ofa nyingine, lakini bado inaendelea kumfuatilia kiungo huyo wa England.
Wakati huohuo, bado haijafahamika kama City iko tayari kufikia thamani iliyowekwa na Chelsea, hasa ikizingatiwa kuwa klabu hiyo pia inamfuatilia kiungo wa Lille raia wa Morocco, Ayoub Bouaddi.
Pia, Manchester City imeanza kuangalia kuhusu uwezekano wa kumsajili beki wa Chelsea, Malo Gusto.
Chelsea iko tayari kumuuza beki huyo wa kulia kufuatia kuwasili kwa Marco Palestra kutoka Atalanta, lakini imemuwekea bei ya pauni75 milioni.