Msomalia aweka historia, PSG yateteza taji
Muktasari:
- Mwamuzi Artan ambaye alizuiwa kuingia Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la mwaka huu, sasa ameweka historia mpya katika michuano ya ngazi ya juu barani Ulaya.
SALZBURG, AUSTRIA: MWAMUZI Msomalia, Omar Artan ameandika historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Afrika kuchezesha UEFA Super Cup ambayo Paris Saint-Germain (PSG) imetetea taji la UEFA Super Cup baada ya kuichapa Aston Villa kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Red Bull Arena, Salzburg.
Mwamuzi Artan ambaye alizuiwa kuingia Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la mwaka huu, sasa ameweka historia mpya katika michuano ya ngazi ya juu barani Ulaya.
Katika mchezo huo mshambuliaji Desire Doue ndiye aliyeipa PSG ushindi baada ya kufunga bao la pili dakika ya 62, huku bao hilo likikaguliwa na mfumo wa VAR kutokana na tuhuma za kuotea kabla ya kuthibitishwa kuwa halali.
PSG ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 20 kupitia Khvicha Kvaratskhelia, aliyepiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Hata hivyo, Aston Villa ilisawazisha dakika ya 45 kupitia kinda Brian Madjo, aliyefunga kwa ustadi na kuandika historia kwa kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Super Cup.
Madjo, mwenye umri wa miaka 17 na ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya England chini ya miaka 17, alifunga katika mchezo wake wa kwanza kwenye Red Bull Arena.
Kabla ya kupata bao hilo, Madjo alikuwa amepoteza nafasi mbili nzuri, akipiga shuti nje na baadaye kupiga kichwa kilichokwenda juu ya lango. Hata hivyo, alijibu kwa staili alipounganisha kwa voleya krosi ya John McGinn kwenye dakika za mwisho za kipindi cha kwanza.
Bao hilo lilikuwa hitimisho zuri la mapambano ya miezi minane ya Madjo kutaka kucheza mechi za ushindani, baada ya Villa kuzuiwa na FIFA kumsajili kwenye mashindano kufuatia uhamisho wake kutoka Metz kwa ada ya pauni milioni 10 mwezi Januari.
Villa ilishinda rufaa mwanzoni mwa Agosti kupitia Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), iliyomruhusu Madjo kucheza mechi za ushindani.
Kinda huyo alikuwa tishio kubwa kwa safu ya ulinzi ya PSG kutokana na nguvu zake, lakini bao lake halikutosha kuizuia timu hiyo ya Ufaransa kutetea taji ililolibeba kwa mara ya kwanza mwaka jana baada ya kuifunga Tottenham kwa penalti.
Aston Villa, iliyoshiriki Super Cup baada ya kutwaa Europa Ligi mwezi Mei, ilipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini kipa wa PSG, Matvey Safonov, alifanya kazi nzuri kuokoa mashambulizi hayo.
Kufuatia kipigo hicho, kocha wa Villa, Unai Emery, amepoteza fainali zote nne za UEFA Super Cup alizoshiriki, ikiwa ni pamoja na zile alizowahi kucheza akiwa na Sevilla na Villarreal.