Mtanzania aibeba Australia Kombe la Dunia
Muktasari:
- Irankunda ameifanya Australia kuanza vizuri fainali za Kombe la Dunia kufuatia bao alilofunga wakati timu hiyo ya taifa ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa BC Place, Vancouver.
VANCOUVER, CANADA: WAKATI mashabiki wengi wa soka wakiwatazama nyota wakubwa wa Uturuki kama vile Arda Guler na Kenan Yıldız, kijana mwenye asili ya Tanzania, Nestory Irankunda, amefanya yake baada ya kuifungia Australia bao muhimu katika mchezo wa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya timu hiyo.
Irankunda ameifanya Australia kuanza vizuri fainali za Kombe la Dunia kufuatia bao alilofunga wakati timu hiyo ya taifa ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa BC Place, Vancouver.
Katika mchezo huo, Australia iliingia uwanjani ikiwa haipewi nafasi kubwa mbele ya Uturuki ambayo iliongozwa na nyota wake wanaocheza ligi kubwa za Ulaya, akiwemo Guler anayekipiga Real Madrid.
Hata hivyo, Irankunda alibadili upepo kwa kutumia kasi yake na kuipa uongozi timu hiyo katika dakika 27 kufuatia asisti ya Okon-Engstler.
Licha ya muda mwingi kuwa nyuma kutokana na mashambulizi mfululizo ya Uturuki, Australia ilionekana kucheza kwa nidhamu kubwa huku ikiziba mianya yote kitu ambacho kiliwafanya wapinzani wao kuwa na wakati mgumu kuwafungua katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Katika dakika ya 65, kocha wa Australia Tony Popovic aliamua kufanya mabadiliko ya kwa kumtoa Irankunda na kuingia Nishan Velupillay ili kuongeza nguvu zaidi kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji baada ya kazi kubwa iliyofanywa na kijana huyo.
Wakati wakisaka bao la kusawazisha, Uturuki ilijikuta ikiruhusu bao la pili ambalo walifungwa na Connor Metcalfe katika dakika 75 na kuifanya A Australia kuanza vizuri fainali hizo.
Kwa miaka kadhaa sasa, Irankunda amekuwa akitajwa kama moja ya vipaji bora vilivyozalishwa na Australia. Alijitengenezea jina akiwa na klabu ya Adelaide United kabla ya kuvutia vigogo wa Ulaya na kupata nafasi ya kuhamia kwa mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich.
Uhamisho wake kwenda Bayern Munich ulionekana kama hatua kubwa katika maendeleo yake huku makocha na wachambuzi wengi wakiamini ana kila sifa za kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa duniakatika miaka ijayo. Ana kasi, nguvu, uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na kujiamini anapokuwa na mpira miguuni.
Nyota huyo ambaye kwa sasa anaichezea Watford, alizaliwa Kigoma, Tanzania, ndani ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu baada ya wazazi wake kukimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.
Waaliishi Tanzania kwa muda kabla ya kupata hifadhi nchini Australia, ambako Irankunda alianza safari yake ya soka iliyomfikisha kucheza katika ngazi ya juu barani Ulaya na sasa kuandika historia katika Kombe la Dunia.
Kutoka kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu hadi kufunga bao kwenye michuano mikubwa zaidi ya soka duniani, safari ya Irankunda ni ushuhuda kwamba ndoto zinaweza kutimia bila kujali mtu ametoka wapi.