Irankunda aondoka Watford, ajiunga Sporting
Muktasari:
- Irankunda, mwenye umri wa miaka 20, alijiunga na Watford Julai 2025 akitokea Bayern Munich, lakini ameshindwa kudumu kwa muda mrefu Vicarage Road.
LONDON, ENGLAND. MSHAMBULIAJI wa Watford, Nestory Irankunda, ameondoka klabuni hapo baada ya msimu mmoja na kujiunga na vigogo wa Ureno, Sporting Lisbon, kwa uhamisho wa moja kwa moja.
Irankunda, mwenye umri wa miaka 20, alijiunga na Watford Julai 2025 akitokea Bayern Munich, lakini ameshindwa kudumu kwa muda mrefu Vicarage Road.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Australia alifunga mabao manne katika mechi 44 alizoichezea Watford kabla ya kuamua kuhamia Sporting. Uhamisho huo unasubiri kukamilishwa kwa taratibu za kupata kibali cha kimataifa.
Licha ya kutokuwa na msimu wenye kiwango kikubwa katika klabu, Irankunda aling'ara akiwa na timu ya taifa ya Australia, akifunga mabao matano msimu uliopita.
Miongoni mwa mabao hayo ni lile la kwanza la Australia katika Kombe la Dunia, wakati Socceroos ilipoifunga Uturuki mabao 2-0.
Bao hilo lilimfanya Irankunda kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwa Australia katika historia ya Kombe la Dunia, rekodi iliyoongeza thamani yake kwenye soko la uhamisho.
Sasa Irankunda anahamia Sporting Lisbon akiwa na matumaini ya kufufua kiwango chake na kujijengea nafasi katika moja ya klabu kubwa nchini Ureno.