Sunderland yamsajili Methalie kwa Sh68 bilioni
Muktasari:
- Klabu hizo zimefikia makubaliano ya awali ya pauni milioni 23.9, huku pauni nyingine milioni 1.7 zikitarajiwa kulipwa kama bonasi kulingana na utendaji wa mchezaji na masharti ya mkataba.
SUNDERLAND, ENGLAND: SUNDERLAND imefikia makubaliano ya kumsajili beki wa kushoto wa Toulouse, Dayann Methalie, kwa ada ya jumla ya pauni milioni 25.6, sawa na takribani Sh68 bilioni.
Klabu hizo zimefikia makubaliano ya awali ya pauni milioni 23.9, huku pauni nyingine milioni 1.7 zikitarajiwa kulipwa kama bonasi kulingana na utendaji wa mchezaji na masharti ya mkataba.
Methalie, mwenye umri wa miaka 20, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Sunderland.
Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa alicheza mechi 28 za Ligue 1 msimu uliopita akiwa na Toulouse, akifunga mabao mawili katika mechi zake tatu za mwisho.
Toulouse ilimaliza msimu huo ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligue 1, huku kiwango cha Methalie kikimfanya kuvutia Sunderland katika dirisha hili la usajili.