Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SUPER SUNDAY: Simba baada ya Dabi, Arsenal v Man City...

Muktasari:

  • Sasa ni rasmi kuanzia jana, mambo yameanza kuchangamka, kila timu imeonekana kuwa tayari kuuanza msimu mpya, Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, mambo yalianza kwa mechi tatu kupigwa Ijumaa,

KWA mashabiki wa soka, ni sahihi kusema wamepata shida kidogo sana kipindi hiki, baada ya misimu kumalizika, macho na masikio yao yaligeukia kwenye michuano ya Kombe la Dunia, ubishi ulikuwa mwingi, mashabiki wakawa wanajazana vibanda umiza usiku mnene, hatimaye mwisho Hispania ikatwaa ubingwa huo.

Sasa ni rasmi kuanzia jana, mambo yameanza kuchangamka, kila timu imeonekana kuwa tayari kuuanza msimu mpya, Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, mambo yalianza kwa mechi tatu kupigwa Ijumaa, jana kukawa na mechi nyingine, wale wanetu tayari wameanza kuokota vibunda, lakini mambo makubwa ni leo siku ambayo Mwanaspoti wameibatiza kwa jina la ‘SUPER SUNDAY’ kukiwa na mechi kali, Ulaya, Afrika pamoja na Tanzania. Kila mmoja macho ni uwanjani.

Ni muendelezo wa ligi kadhaa Ulaya ikiwemo La Liga, ni fainali ya WAFCON mashindano ambayo yamekuwa na msisimko mkubwa sana kwa mwaka huu, ni mechi za Ligi Kuu Bara, lakini kumbuka kuwa kuna mchezo mkali wa Ngao ya Jamii kati ya Manchester City mpya ikivaana na Arsenal ya zamani. Twende wote.


SIMBA BAADA YA DABI

Klabu ya Simba inafungua pazia la Ligi Kuu Bara leo ugenini kucheza dhidi ya kikosi cha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, ikiwa ni kibarua kingine kigumu kwa kocha wa timu hiyo, Steve Barker, baada ya kukosa Ngao ya Jamii.

Simba inaanza kampeni hiyo ikiwa ni siku nne zimepita tangu ikose taji la Ngao ya Jamii kwa kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Yanga katika mechi ya ‘Kariakoo Derby’, iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar Agosti 12, 2026.

Mechi hii itakayopigwa saa 12:00 jioni, Simba inakutana na Kagera Sugar iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, ikiungana na maafande wa Polisi Tanzania na mabingwa wa Ligi ya Championship, Geita Gold iliyomaliza ikiwa vinara.

Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri mara ya mwisho ilipocheza kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kwa sababu iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-2, Desemba 21, 2024, ikiwa ni kipigo kikubwa cha msimu wa 2024-2025.

Katika mechi hiyo, mabao ya Simba yalifungwa na Shomari Kapombe dakika ya 13, Jean Charles Ahoua dakika ya 44, Fabrice Ngoma dakika ya 54 na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho Mganda Steven Mukwala akifunga mawili dakika ya 67 na 85.

Kwa upande wa mabao ya Kagera Sugar katika mechi hiyo, yalifungwa na beki wa kulia, Datius Peter dakika ya 80 na kiungo Cleophace Mkandala dakika ya 90+3 na sasa kikosi hicho kina kazi nyingine ngumu ya kuhakikisha kinalipa tena kisasi.

Mbali na hilo, ila Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa na rekodi bora katika Ligi Kuu Bara, kwani hadi sasa kikosi hicho hakijapoteza, tangu mara ya mwisho kilipochapwa mabao 2-0 na Azam FC, Desemba 7, 2025.

Katika mechi hizo 25, ilizocheza Simba za Ligi Kuu Bara bila kupoteza imeshinda 18 na kutoka sare saba, huku ikifunga jumla ya mabao 43 na kuruhusu pia manane, unawezekana kuwa mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa Simba ili kuona kikosi chao kama kina maboresho makubwa tofauti na kile kilichochapwa na Yanga, lakini kwa mashabiki wengine ni nafasi kwao kuona Juma Kaseja ambaye ni kocha wa Kagera na mchezaji wa zamani wa Simba atakujaje kwenye mchezo huu wa kwanza kwake nyumbani msimu huu.

Endapo Simba itashindwa kupata ushindi kwenye mechi hii, presha kubwa itaanza kwa kocha wa timu hiyo Steve Barker kwani utakuwa mchezo wa pili mfululizo anashindwa kuibuka na ushindi


MBWENI KUNA BURUDANI

Mechi nyingine ya Ligi leo itapigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini, Dar es Salaam, ambapo wenyeji maafande wa JKT Tanzania watakuwa na kibarua kigumu cha kuanza msimu wa 2026-2027, kwa kupambana dhidi ya TRA United.

Mechi hiyo itakayopigwa saa 2:30 usiku, inazikutanisha timu zote zilizofanya vizuri msimu wa 2025-2026 na JKT Tanzania ilimaliza nafasi ya sita na pointi 42, ikizidiwa moja tu na TRA United iliyoshika ya tano na pointi 43.

JKT inaingia na rekodi bora ya kutopoteza mechi dhidi ya TRA United kwa msimu wa 2025-2026 na ilianza kwa ushindi ikicheza nyumbani wa bao 1-0, Novemba 26, 2025, kisha ugenini ikatoka sare ya kufungana bao 1-1, Mei 12, 2026.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema maandalizi yamekamilika kwa kiwango kikubwa na wako tayari kwa ushindani huo, huku Kocha Mkuu wa TRA United, Etienne Ndayiragije akijivunia usajili wa wachezaji wapya akiamini kuwa wanaweza kuibeba timu yake ili kutimiza lengo la kumaliza kwenye nne bora msimu huu.


WABABE ENGLAND WANAKUTANA

Majira ya saa 11:00 jioni mashabiki wa Arsenal wataanza maneno yao waliyomaliza nayo msimu uliopita wakati ambapo chama lao litakuwa uwanjani kuvaana na Manchester City kwenye mchezo mkali wa Ngao ya Jamii, ambayo inachukuliwa kama ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu England itakayoanza baadaye wiki hii.

Arsenal msimu uliopita ilimaliza kibabe baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England mbele ya Man City ikiwa ni mara ya kwanza inafanya hivyo baada ya kupita miaka 22.

Huu ni mchezo wenye sura tofauti na ile ya msimu uliopita ambapo Arsenal inakwenda ikiwa na maongezo ya wachezaji wawili tu kwenye kikosi chake, huku City ikiwa na kundi kubwa la mastaa wapya lakini pia kocha Enzo Maresca ni mgeni kwenye timu hiyo akiwa amechukua nafasi ya Pep Guardiola ambaye aliachana na timu hiyo baada ya msimu kumalizika.

Baada ya miaka mingi mchezo huu unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Principality jijini Cardiff badala ya Wembley sehemu ambayo mechi hizi zimekuwa zikipigwa kwa miaka mingi.

Hata hivyo, uwanja huu una bahati kwa Arsenal kwani imecheza mechi 10 na kushinda mataji manne ya Ngao ya Jamii huku Man City ikicheza hapo mchezo mmoja tu wa kufuzu UEFA dhidi ya TNS na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kila timu inafahamu kuhusu uwanja huo.


LA LIGA MAMBO SAFI

Kwa wale wapenzi wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga mambo yameanza na leo kutakuwa na mechi mbili kali kati ya wenyeji Racing Santander dhidi ya wabishi Villareal kwenye mechi ya unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa ligi hiyo.

Mechi nyingine kali kwenye ligi hiyo itawashuhudia wakongwe Espanyol wakivaana na Levante kwenye mchezo utakaokuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora wa timu zote mbili na usajili ambao zimeufanya kuelekea msimu huu wa ligi.

Espanyol na Levante zimekutana mara 46 zikiwa ni kati ya timu kwenye ligi hiyo ambazo zimekutana mara nyingi zaidi, hata hivyo, Espanyol ndiyo wanaongoza kwa kupata ushindi wakiwa wameshinda mechi 19 huku Levante wakishinda michezo kumi.

Wakiwa kwenye Uwanja wa RCDE, Espanyol wana faida kubwa wakiwa wamepata ushindi hapo mara 13 kati ya michezo 23 waliyokutana, huku Levante wakiwa wamepata ushindi mara tatu.

Racing hawajashiriki Ligi Kuu ya Hispania tangu msimu wa 2011-12, na tangu wakati huo wametumia muda katika daraja la tatu, lakini walitwaa ubingwa wa Segunda Division msimu wa 2025-26 na hivyo kupata nafasi ya kurejea La Liga kwa msimu mpya.

Kikosi cha Jose Alberto kilicheza mechi sita za kirafiki za maandalizi ya msimu na kiliweza kushinda mchezo mmoja pekee kati ya hiyo, uliokuwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Sporting Gijon Agosti 7.

Racing wana michezo mitatu ya La Liga kabla ya mwisho wa Agosti, wakisafiri kwenda Getafe baada ya mchezo huu kabla ya kumaliza mwezi wakiwa nyumbani dhidi ya Elche.

Timu hii imekutana na Villarreal mara 33 hapo awali na wamefanikiwa kupata ushindi mara nane pekee, lakini walishinda katika mechi yao ya mwisho kwa ushindi wa 2-1 katika hatua ya 32 bora ya Copa del Rey msimu uliopita, huu ni mchezo mkali sana, lakini unaweza kuwa wa upande mmoja.


MUDA WA CHAKULA CHA USIKU

Leo saa 2:00 usiku katika Dimba la Moulay El Hassan mjini Rabat, Morocco itakwenda kushuhudiwa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) baada ya kusubiri kwa siku 21 kati ya Malawi na Cameroon. Hii itakuwa mechi ya historia na heshima kwenye soka la wanawake barani Afrika.

Ni fainali ya kipekee kwa sababu Malawi, ambayo ni mara yake ya kwanza kushiriki fainali hizo, imefika hatua ambayo hata mataifa yenye historia kubwa yalishindwa kufika.

Hii ni fainali ya 14 ya mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1991 wakati huo yakijulikana kama Michuano ya Afrika kwa Wanawake (African Womens Championship) kabla ya kubadilishwa jina mwaka 2015 na kuitwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake.

Katika mashindano hayo Nigeria ndio timu pekee iliyocheza fainali nyingi ikicheza 10 na kushinda mataji 10 (1998,2000

2002, 2004, 2006, 2010, 2014, 2016, 2018, 2024), Equitorial Guinea (2008,2012), ikitwaa mataji mawili na Afrika Kusini taji moja (2022).

Ni mchezo uliojaa hisia kali kwa mashabiki, lakini ni pigo kubwa kwa Morocco ambao watalazimika kujaa uwanjani kuwashangilia wanawake kutoka kwenye mataifa mengine baada ya timu yao kushindwa kufika fainali.

Kabla hujala chakula cha usiku, tazama mechi hii kali na ya kihistoria kwenye soka la Wanawake.