Rais Samia ampongeza bingwa wa gofu
Muktasari:
- Wanyeche aliibuka mshindi katika mashindano hayo yaliyoshirikisha wachezaji kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo Uganda, Ghana, Japan, Kenya, Nigeria, Rwanda na Tanzania.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemtumia salamu za pongezi kwa mchezaji wa Klabu ya Gofu Lugalo, Hawa Wanyeche, baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya Uganda Ladies Open.
Wanyeche aliibuka mshindi katika mashindano hayo yaliyoshirikisha wachezaji kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo Uganda, Ghana, Japan, Kenya, Nigeria, Rwanda na Tanzania.
Kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Rais Samia alisema ushindi huo umeiletea heshima Tanzania na kuthibitisha uwezo wa wanamichezo wa ndani kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Ushindi huu ni fahari kubwa kwa Taifa letu na unaonesha uwezo wa wachezaji wetu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuendeleza sekta ya michezo nchini kwa kuweka mazingira wezeshi na kuboresha miundombinu ili wanamichezo waweze kutimiza malengo yao na kuiwakilisha Tanzania kimataifa.
Ushindi wa Wanyeche unaongeza chachu katika mafanikio ya michezo nchini, huku gofu likizidi kuonyesha uwezo wake katika kuiwakilisha Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa.
Mafanikio hayo yanakuja siku chache baada ya Rais Samia kuwapongeza pia mabingwa wa soka, Yanga, hatua inayoonyesha kuendelea kupewa kipaumbele kwa michezo mbalimbali nchini.