Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msomali wa Kombe la Dunia apewa fainali Kagame

Muktasari:

  • Kilele cha mashindano hayo kinatarajiwa kuwa Agosti 7, 2026 kwenye Uwanja wa Amahoro, ambapo bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati atatawazwa.

BAADA ya mapumziko ya siku mbili kufuatia kumalizika kwa hatua ya makundi ya Kombe la CECAFA Kagame 2026, mechi za nusu fainali zitapigwa Jumanne hii huku maandalizi ya fainali yakianza kushika kasi jijini Kigali.

Kilele cha mashindano hayo kinatarajiwa kuwa Agosti 7, 2026 kwenye Uwanja wa Amahoro, ambapo bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati atatawazwa.

Katika kuhakikisha mchezo huo unakuwa wa kiwango cha juu, CECAFA imemteua mwamuzi wa kimataifa kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan, kuwa mwamuzi wa fainali hiyo.

Artan, ambaye mwaka 2025 alitajwa kuwa mwamuzi bora wa wanaume wa CAF, atakuwa akiongoza mchezo huo akiwa na wasaidizi wake wawili, Liban Abdulrazack kutoka Djibouti na Eliezer Stephen Yiembe wa Kenya.

Uteuzi huo umeongeza uzito wa fainali hiyo kutokana na heshima ambayo Artan amejijengea ndani ya Afrika na kimataifa huku wiki chache zilizopita akiwa gumzo wakati wa Kombe la Dunia 2026 kufuatia Marekani kumgomea kuingia nchini humo kwa ajili ya kucheza fainali hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa CECAFA, Jean Sseninde, ndiye aliyetangaza uteuzi huo, akieleza kuwa uwepo wa Artan ni sehemu ya kuonyesha ubora na viwango ambavyo taasisi hiyo inalenga kuvifikia.

Rais wa CECAFA, Paulos Weldehaimanot Andemariam, amesema kurejea kwa Artan kwenye ukanda huu ni heshima kubwa kwa mashindano hayo.

“Artan amekuwa alama ya ubora katika uamuzi wa soka Afrika. Mafanikio yake yanaendelea kuwa chanzo cha hamasa kwa waamuzi wengine,” alisema.

Mbali na kuchezesha fainali ya Kagame Cup, Artan na wasaidizi wake watatumia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa UEFA Super Cup utakaochezwa Agosti 12, 2026 jijini Salzburg, Austria, kati ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain, dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Europa, Aston Villa.

NNE ZAPIGANIA TIKETI YA FAINALI

Kabla ya kufika kwenye mchezo wa kuwania taji, timu nne zimebakiza hatua moja kuelekea fainali baada ya kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi.

Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Jamus ya Sudan Kusini na Al Hilal ya Sudan ndizo zimeingia hatua ya nusu fainali inayotarajiwa kupigwa leo.

Mwenyeji Rayon Sports ndiyo timu iliyokuwa na rekodi bora zaidi katika hatua ya makundi baada ya kushinda mechi zote tatu na kukusanya pointi tisa.

Rayon ilianza kwa kuifunga KVZ ya Zanzibar mabao 2-0, ikaendelea kuifunga Tusker ya Kenya bao 1-0 kabla ya kumaliza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal.

Sasa miamba hiyo ya Rwanda itakutana na Jamus ya Sudan Kusini katika nusu fainali, pambano ambalo limepewa uzito kutokana na namna timu hiyo ilivyovuruga mipango ya waliokuwa wakipewa nafasi kubwa.

Jamus ilishangaza wengi baada ya kuifunga Singida Black Stars mabao 2-0, bingwa mtetezi wa mashindano hayo na baadaye kutoa suluhu dhidi ya Simba kabla ya kuichapa Mogadishu City mabao 2-1.

Kwa upande mwingine, Al Hilal itakutana na Gor Mahia katika nusu fainali nyingine, mchezo unaotarajiwa kuwa wa ushindani kutokana na historia na uzoefu wa timu hizo katika mashindano ya kimataifa.

Al Hilal ilitinga hatua hiyo baada ya kumaliza ikiwa miongoni mwa timu bora zilizoshika nafasi ya pili, huku Gor Mahia ikiingia kama kinara wa kundi lake.

UBINGWA NA MKWANJA MEZANI

Mbali na heshima ya kutwaa taji la CECAFA Kagame Cup, timu zitakazofika hatua ya mwisho pia zinawania zawadi ya fedha.

Bingwa wa mashindano hayo ataondoka na dola 30,000 (Sh79.3 milioni), mshindi wa pili atapata dola 20,000 (Sh52.8) huku mshindi wa tatu akipewa dola 10,000 (Sh26.4 milioni).

Kwa Rayon Sports, fainali hiyo inaweza kuwa nafasi ya kipekee kutwaa ubingwa mbele ya mashabiki wake wa nyumbani.

Kwa Jamus, itakuwa nafasi ya kuendeleza simulizi ya timu iliyokuja bila kupewa nafasi kubwa lakini imekuwa moja ya habari kubwa za mashindano haya.

Gor Mahia nayo inatafuta kurejesha heshima yake kwenye michuano ambayo imewahi kuwa na historia kubwa kwake, huku Al Hilal ikitaka kuthibitisha ubora wake kama moja ya klabu kubwa kwenye ukanda wa CECAFA.


WASIKIE WADAU

Kocha wa Bugesera FC ya Rwanda, Musa Gatera, amesema hatua ya nusu fainali itakuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote zilizofuzu.

“Hatua ya makundi imeonyesha kuwa hakuna timu ndogo kwenye mashindano haya, Rayon imeonyesha ubora, lakini Jamus imeonyesha inaweza kushindana na yeyote. Gor Mahia na Al Hilal nazo zina uzoefu mkubwa, hivyo naamini tutashuhudia mechi mbili zenye ushindani mkubwa na zitaamuliwa na makosa madogo,” alisema Gatera.

Kwa upande wake, kocha Mtanzania anayefundisha nchini Rwanda, Baraka Hussein, aliyewahi kuinoa Etincelles FC, amesema ubora ulioonekana tangu hatua ya makundi unaifanya nusu fainali kuwa ngumu kutabirika.

“Rayon Sports ina faida ya kucheza nyumbani na imekuwa na mwendelezo mzuri, lakini kwenye hatua ya mtoano hilo halitoshi. Jamus imeonyesha nidhamu kubwa ya kiuchezaji huku Gor Mahia na Al Hilal zikiwa na uzoefu wa kucheza mechi za presha. Nafikiri tutashuhudia nusu fainali mbili zenye kiwango cha juu,” alisema Baraka.

Baraka aliongeza kuwa uteuzi wa mwamuzi  Artan ni ishara CECAFA inataka fainali ya mwaka huu isimamiwe kwa viwango vya juu vya kimataifa.

“Artan ni mwamuzi mwenye uzoefu mkubwa na amekuwa akisimamia mechi za hadhi ya juu Afrika. Uteuzi wake unaongeza hadhi ya mash indano na unawapa wachezaji na mashabiki imani ya kuona mchezo utache zeshwa kwa ubora.”