Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Salah ageuziwa kibao Liverpool

Muktasari:

  • Mwishoni mwa wiki iliyopita Salah alidai kwamba amekuwa akishambuliwa na kupewa lawama kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika Ligi Kuu England msimu huu.

LIVERPOOL, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Mohamed Salah ameibua mjadala mkali siku chache baada ya kuishambulia timu hiyo na na benchi la ufundi chini ya kocha Arne Slot.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Salah alidai kwamba amekuwa akishambuliwa na kupewa lawama kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika Ligi Kuu England msimu huu.

Wakizungumzia kauli hiyo nyota wa zamani wa timu hiyo, Michael Owen na Jamie Carragher waliodai kwamba kuna jambo halipo sawa katika kikosi hicho na hasa katika masuala ya uhusiano kati ya mchezaji huyo na makocha wake.

"Inawezekana ana doge moyoni. Kimsingi huwezi kutoka kuibeba timu mabegani mwako msimu mmoja, kisha unapoingia msimu mwingine unajikuta benchi, na mbaya zaidi hata kiwango chako hakishawishi," alisema Owen.

Mkongwe huyo aliyewahi kuzichezea pia Manchester United na Real Madrid alisema inawezekana Salah alivimba kichwa msimu uliopita baada ya kuonyesha kiwango bora na hivyo suala la kuwekwa benchi msimu huu limemfanya ahamaki.

"Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu ndiyo maana unapozingua timu inaweza kukufungulia mlango ukaondoka zako hata kama wewe ni bora kuliko wachezaji wenzako kikosini," alisema Owen.

Kwa Carragher aliyewahi kuvaa kitambaa cha unahodha katika kikosi hicho alisema Salah anastahili heshima, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba ni mchezaji kama wengine na anapaswa kuzingatia miiko ya mchezaji wa kulipwa.

"Huwezi kuamka tu na kulalamika, kwani wewe nani? Liverpool ni timu kubwa wampita wachezaji bora pengine hata robo ya uwezo wa baadhi yao huwezi kuufikia. Inamlazimu Salah atulie, ashirikiane na kocha kumaliza tofauti kama zipo," alisema.

Katika maelezo yake, Salah alidai kwamba yeye siyo chanzo cha timu kufanya vibaya na kwamba, kuna sababu basi mchawi labda ni mtu mwingine kwa sababu hahusiki katika mambo yanayohusiana na ufundi.

Mchezaji huyo aliendelea aliendelea kuwekwa benchi katika mechi dhidi ya Leeds United ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3, ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwa Liverpool tangu msimu huu ulipoanza. Mechi hiyo ilikuwa ya tatu mfululizo kwa Salah kukalia benchi, jambo ambalo linaonekana kuanza kumchosha.

Baada ya mchezo, Salah alisema kuna uwezekano mdogo kwake kumalizia maisha yake ya soka katika viunga vya Liverpool akidai kuna mtu anataka yeye ndiyo abebweshe lawama zote juu ya kile kinachoendelea katika timu kwa sasa.

Staa huyo wa kimataifa wa Misri, 33, alisema: “Nimevunjika moyo sana. Nimefanya mambo mengi sana kwa ajili ya klabu hii. Kila mtu ameona hilo kwa miaka yote, hasa msimu uliopita. Inaonekana kama klabu inanigeuka. Ndivyo ninavyohisi.

Ni wazi kabisa kuna mtu anataka lawama zote ziwe juu yangu.”

Licha ya Liverpool kutwaa ubingwa msimu uliopita, msimu huu imekuwa katika hali mbaya ikishuka hadi nafasi ya nane, ikiwa pointi 10 nyuma ya vinara Arsenal. Salah ambaye alifunga mabao 34 katika mashindano yote msimu uliopita na huu ana mabao manne kwenye mechi 13 za Ligi Kuu England.

Hata hivyo, Salah katika mahojiano yake hakuwa muwazi sana juu ya uhusiano wake na kocha aliposema: “Nimesema mara nyingi kuwa nilikuwa na uhusiano mzuri na kocha, lakini ghafla hatuna tena uhusiano wowote. Sijui kwa nini. Hili halikubaliki kwangu… kama ningekuwa sehemu nyingine, klabu ingemlinda mchezaji wake.”

“Inaonekana kama wananishusha katika basi la timu kwa lazima kwa sababu wanaona ndiye tatizo, lakini mimi sioni hivyo. Nimefanya mambo mengi kwa ajili ya klabu hii. Natakiwa kupata heshima ninayostahili.”

“Nimekuwa hapa na nimefunga mabao mengi kuliko mchezaji yeyote wa kizazi hiki. Kwa kweli tangu nimetua kwenye timu hii sidhani kama kuna mtu amefunga mabao mengi kuliko mimi au kutoa asisti nyingi.”

Salah pia alimchana Carragher akisema," Unatoka nyumbani kwenda katika mechi na hujui kama utaanza au la. Kesho utamuona Carragher ananishambulia tena na tena. Sawa tu.”

Salah alienda mbali akilinganisha kinachomtokea na kilichowahi kumkuta Harry Kane  akisema: "Nakumbuka muda fulani Harry Kane alikuwa hafungi kwa karibu mechi 10 akaja kufunga moja au mbili, lakini vyombo vya habari vilisema ‘Ah, Harry atafunga tu’. Kwa Mo, wanataka niwe benchi.”

Mchezaji huyo ambaye hadi sasa amefunga mabao 250 akiwa na Liverpool, alisema tayari amezungumza na kocha kuhusu kuachwa kwake benchi.

“Nilikuwa na kikao na kocha. Anajua hisia zangu. Awali, nilidhani ningeongeza mkataba na kumaliza maisha yangu hapa, lakini mambo hayapo kama yalivyopangwa. Klabu iliniahidi mengi katika dirisha la majira ya kiangazi, lakini nimeanzia benchi katika mechi tatu. Nachoweza kusema ni kwamba watimize ahadi.”

Liverpool ilitarajiwa kucheza na Inter Milan katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana Jumanne, kisha itarudi katika ligi kucheza dhidi ya Brighton Jumamosi ambayo inaweza kuwa mechi ya mwisho ya Salah kabla hajajiunga na timu ya taifa ya Misri kwa ajili ya Afcon nchini Morocco wiki ijayo.

“Nitakuwa Anfield, kuwaaga mashabiki, kisha nitaenda Afcon. Sijui nini kitatokea nikiwa kule.”

Kocha Slot alieleza kwa nini alimuacha Salah benchi kwenye mechi dhidi ya Leeds akisema: "Tulikuwa tunaongoza 2-0, kisha 3-2 ilikuwa muhimu zaidi kudhibiti mchezo. Hatukuhitaji bao. Kwa kawaida tukihitaji bao kama wiki iliyopita dhidi ya Sunderland huwa namuingiza Mo.”