Messi afuata nyayo za Ronaldo, anunua klabu Hispania
Muktasari:
- Kwa kununua klabu hiyo, Messi ameimarisha zaidi uhusiano wake na eneo la Catalonia, ambako aliwahi kujijengea jina kubwa akiwa Barcelona. Hata hivyo, kurejea kwake kucheza Barcelona bado kunaonekana kuwa jambo gumu kutokana na mkataba wake wa sasa na Inter Miami inayomilikiwa na David Beckham hadi mwaka 2028.
BARCELONA, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Barcelona, Lionel Messi, ameanza rasmi safari ya uwekezaji katika soka kwa kununua asilimia 100 ya klabu ya daraja la tano nchini Hispania, UE Cornella, iliyopo umbali wa takriban kilomita 10 kutoka jijini Barcelona.
Nyota huyo wa Inter Miami, 38, sasa atakuwa na udhibiti kamili wa klabu hiyo, hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya maisha yake baada ya kustaafu soka la ushindani. Hata hivyo, haijawekwa wazi kiasi cha fedha alichotumia kuinunua timu hiyo, lakini tayari hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa katika ulimwengu wa soka.
Ununuzi huo unakuja wiki chache baada ya mpinzani wake wa muda mrefu, Cristiano Ronaldo, kuanza hatua zake za uwekezaji kwa kumiliki asilimia 25 ya hisa za klabu ya UD Almeria, hivyo kuongeza ushindani wao hata nje ya uwanja.
Kupitia taarifa rasmi, UE Cornella ilieleza ujio wa Messi unaashiria mwanzo wa zama mpya katika historia ya klabu hiyo, ukilenga kuimarisha maendeleo ya kimichezo na kiutawala, huku pia ikiweka mkazo katika kukuza vipaji vya vijana katika akademi yake maarufu.
Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1951, kwa sasa inashiriki ligi ya Tercera Federacion (daraja la tano) na ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na alama 55, nyuma ya Manresa na Badalona, huku ikipambana kuhakikisha inapanda daraja kwenda Segunda RFEF.
UE Cornella inajivunia kuwa moja ya vituo muhimu vya kulea vipaji nchini Hispania, ikiwa imezalisha wachezaji kadhaa waliokuja kuwa nyota wakubwa, wakiwemo kipa wa Arsenal, David Raya, pamoja na beki wa zamani wa Barcelona na Inter Miami, Jordi Alba.
Wengine waliopitia katika mfumo huo ni pamoja na Javi Puado, Keita Balde, Aitor Ruibal na Ilie Sanchez, ambao wote wamefanya vizuri katika ngazi za juu za soka Ulaya na duniani.
Kwa kununua klabu hiyo, Messi ameimarisha zaidi uhusiano wake na eneo la Catalonia, ambako aliwahi kujijengea jina kubwa akiwa Barcelona. Hata hivyo, kurejea kwake kucheza Barcelona bado kunaonekana kuwa jambo gumu kutokana na mkataba wake wa sasa na Inter Miami inayomilikiwa na David Beckham hadi mwaka 2028.