Prime
Hii Dabi hakuna kisingizio, ‘sebene’ litapigwa hapa!
KUNA dakika 90 za moto leo hapa Zanzibar na macho ya wengi yatakuwa Uwanja wa New Amaan Complex, itakapopigwa mechi kubwa kati ya Yanga dhidi ya Simba kuwania taji la kwanza msimu huu la Ngao ya Jamii.
Timu hizo mbili zitakutana kwenye mechi ambayo inaweza kuwa na visasi vingi vya rekodi na utamu zaidi ni hakuna sare lazima mmoja aondoke na kilio mwisho wa mechi.
Simba ilikuwa ya kwanza kufika Zanzibar mapema juzi asubuhi, ikitumia usafiri wa ndege ya Shirika la Tanzania kisha usiku wa siku hiyo ikapasha kwenye uwanja mdogo nje ya Amaan.
Yanga ikafuata nyuma siku hiyo hiyo mchana, ikatua, ikitumia usafiri wa maji kwa kutumia boti za tajiri wa mpinzani wao Azam, Said Bakhresa ikafanya mazoezi jioni pembeni kidogo ya uwanja mwingine mdogo ya ule walioutumia Simba.
Yanga ndio bingwa mtetezi wa taji hili akilitwa msimu uliopita Septemba 16,2025, ilipoichapa Simba bao 1-0 likifungwa na kiungo Pacome Zouzoua dakika ya 56 ambaye leo na msimu ujao kwa jumla hatakuwepo kutokana na majeraha.
Simba ndiyo timu iliyochukua taji hili mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mara 10 na kama italichukua leo itakuwa ya 11, baada ya mwaka 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019, 2020 na mara ya mwisho ikilichukua 2023 ikiifunga Yanga kwa penalti Mkoani Tanga.
Yanga inafuata kwa kuchukua taji hilo mara nane na ushindi leo utaipa la tisa baada ya kulibeba mwaka 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022 na 2025.
Msimu uliopita, timu hizi mbili zilikutana Uwanja wa Amaan mara mbili na mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara ilimalizika kwa suluhu, Yanga ikiwa mwenyeji na zikakutana kwenye Fainali ya Kombe la Muungano na Simba kushinda bao 1-0, hivyo, Yanga itataka kulipa kisasi mbele ya Mnyama.
Mechi hii itakuwa ya tatu kwa Kocha Steve Barker ambaye katika mbili za mwishi ameshinda moja na sare moja na sasa anatafuta ushindi wa pili.
Katika kikosi hicho, sura za nyota wenyeji walioipa mafanikio msimu uliopita kwa kuchukua mataji mawili ni wegi kuliko wapya na hivyo Kocha Berker atahitajinutulivu katika kuamua nani aanze naye.
Yanga chini ya Kocha Manqoba Mngithi atakuwa na dakika 90 za kwanza dhidi ya Simba akisubiriwa kuonyesha kama atamaliza ubabe wa Barker ambaye amekuwa hafungiki kirahisi katika mechi kubwa kama hii.
Barker anataka kuona Simba inacheza soka la kasi na kushambulia kwenda kwa mpinzani huku kukiwa na nidhamu kubwa ya kujilinda na kuutafuta mpira, falsafa itakayokuwa silaha kubwa dhidi ya Yanga
Manqoba atakuwa na kibarua kizito cha kuamua aanze na mastaa gani Yanga na anatengeneza kikosi cha kumpa mafanikio msimu ujao ikiwamo kutetea taji hilo.
Kupata utulivu Manqoba anaweza kutumia mastaa wengi ambao wanajua presha ya mechi kubwa hiyo na wale wapya wengi akiwaanzisha benchi ili kuipa timu utulivu kwenye mechi hiyo.
Makocha hawa wawili wanajuana vyema wakiwa raia wa Afrika Kusini na kabla ya kukutana nchini wamewahi kukutana kwao wakiwa na klabu tofauti na Barker alikuwa na Stellenbosch huku Manqoba akiifundisha Mamelodi Sundowns.
Timu zote mbili zimetoka kupata mshtuko zikipoteza mechi za kirafiki kwenye kilele cha matamasha yao ya kila mwanzo wa msimu na Simba ililala mbele ya Polisi ya Kenya kwa bao 1-0, kisha Yanga ikafuata kwa kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Aigles du Congo ya kutoka DR Congo.
Hata hivyo, matokeo hayo yakaonekana kama timu hizo zilikuwa zinazugana kwa kucheza soka la kawaida lakini mwishowe, leo itajulikana nani alikuwa na siri nzito dhidi ya mwenzake.
Simba itaingia kwenye mechi hiyo ikimkosa beki na nahodha wake, Shomari Kapombe aliyeumia bega kwenye mashindano ya Kagame, Rwanda ingawa imesafiri naye hadi hapa Unguja huku wekundu hao wanaweza kuamua kumtumia David Kameta ‘Duchu’ au beki wake mpya Nathaniel Chilambo.
Yanga wao ukiondoa wachezaji wake walio nje kwa majeraha ya muda mrefu wengine wako kamili, ukibaki uamuzi wa Manqoba.
Timu zote zitaingia kwenye mechi hiyo zikiwa bado zinaonyesha kutokuwa sawasawa, kutokana na kuwa na muda mchache wa maandalizi ya mwanzo wa msimu mpya ambao utapunguza ubora halisi wa vikosi vyote.
Simba imetoka Rwanda kushiriki Kombe la Kagame huku ikijiandaa na msimu mpya na imecheza mechi tatu dhidi ya Mogadishu City na Jamus zote zikimalizika kwa sare isiyo na mabao, ikishinda mechi ya mwisho dhidi ya Singida Black Stars 2-1 lakini ikatupwa nje ya mashindano.
Mechi hizo angalau ndizo zimeipa nguvu Simba ikiwa na kasi kidogo katika uchezaji wake lakini Yanga yenyewe ikicheza mechi tatu lakini kubwa ni moja dhidi ya Aigles du Congo.
WASIKIE MAKOCHA
Akizungumzia mechi hiyo, Barker alisema maandalizi yamekwenda vizuri na timu ipo tayari kutafuta taji la mapema kuelekea msimu ujao.
“Mpango wetu ni kushinda, ni wazi tulitengeneza nafasi hii baada ya kushinda ubingwa wa Shirikisho CRDB, kama timu tumepata haki hii ya kushiriki mechi hii ya Ngao ya Jamii, tumefanya maandalizi mazuri na kujiweka tayari kuanza msimu kwa hesabu chanya,” alisema Barker.
“Tuna nafasi ya kupata mafanikio ya mapema kwa kuchukua taji hili, Simba ni timu ambayo wakati wote ina hesabu za kuchukua mataji, tupo tayari kuanza kulichukua hili.”
Kwa upande wa kocha wa Yanga, Mngqithi alisema ingawa muda hautoshi kwenye maandalizi ya msimu mpya lakini kikosi chake kipo tayari kwenda kushindana na kuipa Simba maswali magumu.
“Hii itakuwa mechi yangu ya kwanza ya dabi, natamani kuona inakuwaje mechi kubwa kama hii, bahati mbaya timu zote hazijapata muda wa kutosha kujiandaa na mechi hii kutokana na ratiba ya timu zote mbili wikiendi iliyopita,” alisema Manqoba.
“Tumekuja hapa kuwapa Simba maswali magumu kwa kushinda, haitakuwa rahisi, kikosi kipo tayari kwa mechi, Kila shabiki wa timu hii anatamani kuona tunalinda mataji yetu, nafahamu Simba ina wachezaji wazuri Mpanzu ( Ellie), Gueye (Lebase), pia wana kiungo raia wa Nigeria aliyekuwa Stellenbosch (Ibraheem Jabaar), kwa hiyo wana timu nzuri.”