Mbeumo na Man United ni kama imeisha!

Muktasari:
- Hilo linaelezwa licha ya Brentford kukataa ofa ya pili ya Pauni 62.5 milioni iliyotumwa na Man United, Ijumaa, lakini bado kuna matarajio makubwa dili likakubalika baada ya kuvuka Jumanne ijayo, ambapo Man United itakuwa imeingia kwenye mwaka mpya wa kifedha baada hesabu za mwaka huu kukomea Juni 30.
MANCHESTER, ENGLAND: BRYAN Mbeumo anaweza kuwa staa mpya wa Manchester United hadi kufikia mwisho wa wiki ijayo, imeelezwa.
Hilo linaelezwa licha ya Brentford kukataa ofa ya pili ya Pauni 62.5 milioni iliyotumwa na Man United, Ijumaa, lakini bado kuna matarajio makubwa dili likakubalika baada ya kuvuka Jumanne ijayo, ambapo Man United itakuwa imeingia kwenye mwaka mpya wa kifedha baada hesabu za mwaka huu kukomea Juni 30.
Hiyo itafanya ada itakayolipwa kwa Mkameruni huyo kuingia kwenye hesabu za mwisho wa msimu ujao. Huko Old Trafford, Mbeumo, 25, atasaini mkataba wa miaka mitano na kulipwa mshahara wa Pauni 180,000 kwa wiki. Man United bado haijapanga tarehe ya vipimo vya afya.
Mbeumo ameziambia Brentford na Tottenham uamuzi wake wa kwenda kujiunga na Man United, kwa mujibu wa The Athletic.
Winga huyo alikuwa kwenye kiwango bora sana msimu uliopita, akifunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England na kuasisti mara saba kuisaidia Brentford kumaliza msimu kwenye nusu ya juu, huku washambuliaji Mohamed Salah, Alexander Isak na Erling Haaland wakiwa pekee ndiyo waliomzidi kwa mabao. Kwa kulinganisha na vinara wa mabao Man United, Bruno Fernandes na Amad Diallo, ambao walifunga mabao manane tu kwenye ligi msimu uliopita.
Kitu cha ziada ni wachezaji wawili tu kwenye Ligi Kuu England ndio waliokimbia au kukabia eneo kubwa msimu uliopita na hivyo kumfanya Mbeumo kuwa mmoja wa mastaa wa moto kabisa.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim anataka kukamilisha usajili wa Mbeumo kwa wakati kabla ya pre-season haijaanza, Julai 7.
Mbeumo mkataba wake huko Brentford unaisha Juni 2026 na kuna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, huku Arsenal, Newcastle na Spurs nazo ziliwahi kuhusishwa na staa huyo.
Ofa ya kwanza ya Man United ilikuwa Pauni 45 milioni pamoja na Pauni 10 milioni ya nyongeza, iligomewa na Brentford kwa sababu wanadai haikufikia kwenye thamani wanayomthaminisha staa huyo. Ofa ya pili ni Pauni 55 milioni na nyongeza ya Pauni 7.5 milioni, nayo pia ilidaiwa kugomewa, lakini mabingwa wa England mara 20 wanaamini watafikia makubaliano.
Spurs ilikuwa na imani ya kumnasa Mbeumo kutokana na uwepo wa kocha wa zamani wa staa huyo, Thomas Frank kwenye kikosi chao, lakini sasa mwenyewe anaonekana kuwa tayari kuhama Gtech Community Stadium kwa ajili ya kwenda Old Trafford tu.
Mbeumo alijiunga Brentford akitokea Troyes ya Ufaransa mwaka 2019 na kipindi hicho timu hiyo ilikuwa kwenye Championship. Amefunga mabao 70 katika mechi 242 alizochezea timu hiyo, ambayo ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu England mwaka 2021.
Man United ina pesa za kumsajili Mbeumo bila hata ya kuhitaji kuuza wachezaji wake, ambapo sasa inaripotiwa mawinga Marcus Rashford, Alejandro Garnacho, Jadon Sancho na Antony wote wamewekwa sokoni. Man United imeshamsajili Matheus Cunha kutoka Wolves.