Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbappe atuma onyo kali kwa Messi na Argentina

Muktasari:

  • Nyota huyo amesema timu yake itakuwa tayari kwa vita vingine dhidi ya supastaa na nahodha wa Lionel Messi ambao ni mabingwa watetezi wa dunia walioutwaa mbele ya kina Mbappe 2022 nchini Qatar.

NEW JERSEY, MAREKANI: NAHODHA na mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe tayari ameanza kufikiria kuhusu kile kinachoweza kuwa moja ya simulizi kubwa zaidi za Kombe la Dunia 2026, ikiwa nchi hiyo na Argentina zitakutana tena katika mechi za michuano hiyo mwaka huu.

Nyota huyo amesema timu yake itakuwa tayari kwa vita vingine dhidi ya supastaa na nahodha wa Lionel Messi ambao ni mabingwa watetezi wa dunia walioutwaa mbele ya kina Mbappe 2022 nchini Qatar.

Uwezekano wa kurudiwa kwa fainali ya kusisimua ya Kombe la Dunia 2022 umeendelea kuwa simulizi kwa mashabiki wa soka duniani, ambapo katika fainali hiyo iliyochezwa Qatar, Argentina ilitwaa ubingwa baada ya ushindi wa mikwaju ya penalti, licha ya Mbappé kufunga mabao matatu (hat-trick) katika moja ya mechi bora zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye historia ya Kombe la Dunia.

Na sasa, huku mashindano mapya yakiendelea, mshambuliaji huyo wa Real Madrid ametuma ujumbe wa kujiamini kuhusu uwezekano wa kukutana tena na Argentina.

Kwa mujibu wa mwanahabari, Fabrizio Romano, Mbappe aliulizwa nini kingetokea ikiwa Ufaransa ingekutana na Messi na Argentina katika fainali nyingine ya Kombe la Dunia ambapo jibu lake lilikuwa jepesi: "Tutakuwa na dhamira na njaa ya kushinda, kama kawaida."

Mbappe mwenye umri wa miaka 27 alisisitiza kuwa lengo la Ufaransa siyo kufika mbali tu kwenye mashindano hayo, bali kuandika historia mpya.

"Tupo hapa kuandika historia. Bado hatujafanya hivyo. Tunataka Kombe hili la Dunia," alisema

Ufaransa imeingia tena kwenye mashindano ikiwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kikosi chake chenye vipaji vingi, hasa katika safu ya ushambuliaji na Mbappe anaendelea kuwa mhimili mkuu wa timu.

Kwa upande mwingine, Argentina inabaki kuwa moja ya timu imara zaidi katika soka la kimataifa, jambo linalowapa mashabiki matumaini ya kushuhudia pambano jingine kubwa kati ya mataifa hayo mawili.

Ushindani kati ya Mbappe na Messi umekuwa sehemu muhimu ya historia ya kisasa ya soka la kimataifa, ambapo walikutana kwa mara ya kwanza katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2018 na Ufaransa kuiondoa Argentina. Miaka minne baadaye, Messi na Argentina walilipiza kisasi kwa kuifunga Ufaransa katika fainali 2022. Ingawa rekodi ya kukutana kwao katika Kombe la Dunia inaonekana kugawanyika kwa usawa, ushindi wa Argentina ulikuja katika mechi bora zaidi ya zote.

Mbali na ushindani wa mataji, wawili hao pia wanapambana katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Kombe la Dunia ambayo Messi anaingia kwenye mashindano mwaka huu akiwa na mabao 13 Kombe la Dunia na anahitaji manne zaidi ili kumpita Miroslav Klose ambaye anashikilia rekodi ya mabao mengi zaidi katika historia.

Mbappe, kwa upande wake, tayari amefunga mara 12 akiwa amecheza mashindano hayo mara mbili, na anahitaji mabao matano kuvunja rekodi.

Kwa mujibu wa muundo rasmi wa hatua za mtoano ya mashindano ya mwaka huu, Argentina na Ufaransa zitawekwa katika pande tofauti za droo iwapo zitafuzu kutoka katika makundi.

Jambo hilo linamaanisha kwamba haziwezi kukutana katika hatua ya 32 bora, 16 bora, robo fainali wala nusu fainali na hivyo kuna njia moja tu ambayo mashabiki wa soka wanaweza kushuhudia pambano jingine la Mbappe dhidi ya Messi katika Kombe la Dunia 2026.

Ili hilo litokee, Argentina na Ufaransa zitapaswa kushinda mechi zote za hatua za mtoano na kufika fainali kwa mara nyingine. Endapo itatokea, dunia ya soka inaweza kushuhudia marudio ya moja ya fainali bora zaidi kuwahi kuchezwa katika historia ya Kombe la Dunia.