Mbappe atikisa matajiri huko PSG
Muktasari:
PSG iliweka wazi haitaki kumpoteza bure Mbappe, lakini bado haitaki kuchekelea ofa zinaletwa.
PARIS, UFARANSA. LISEMWALO lipo wanasema. Na kama halipo, basi linakuja.
Kinachoelezwa huko Ufaransa ni kwamba supastaa matata kabisa, Kylian Mbappe amewaambia mabosi wa klabu yake ya Paris Saint-Germain kwamba anataka kuondoka.
Hilo linasemwa wakati mkali huyo wa kimataifa wa chama la Les Bleus akihusishwa na miamba ya soka ya Hispania, Real Madrid.
Mbappe, 22, mkataba wake kwenye kikosi hicho cha PSG utafika tamati mwakani na haonekani kabisa kuwa na dalili ya kusaini dili jipya la kuendelea kukipiga kwenye timu hiyo inayonolewa na Mauricio Pochettino.
PSG iliweka wazi kwamba haitaki kumpoteza bure Mbappe, lakini bado haitaki kuchekelea ofa zinaletwa kwenye timu hiyo kwa ajili ya kutaka saini ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia.
Lakini, kwa sasa Mbappe amewaambia miamba hiyo ya Ligue 1 anataka kuondoka, kwa mujibu wa RMC Sport – huku mchezaji mwenyewe akivutiwa na mpango wa kwenda kukipiga Santiago Bernabeu.
Mwandishi wa RMC Sport, Daniel Riolo alifichua: “Nafahamu kwamba Mbappe ameomba kuondoka.
“Inachanganya kwa sababu kwanza inakupasa kutafuta klabu yenye pesa inayotoka kumlipa mchezaji huyo.
“Lakini, habari ni kwamba hataki kubaki – kwa sababu mchezaji mwenyewe haamini mipango ya Leonardo.
“Kama hataondoka kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, atakuwa mchezaji huru msimu ujao – na huko Doha (kwa wamiliki wa PSG) hawataki kabisa kusikia hicho kitu.
“Kama Mbappe ataendelea kushikilia msimamo wake kwamba anataka kuondoka, hiyo ina maana PSG italazimika kutafuta timu itakayokuwa tayari kulipa ada inayofaa kumuuza mchezaji huyo na pia itafuta mbadala wake.
“Lakini, ukweli ndio huo, Mbappe hana mpango wa kubaki PSG.”
Los Blancos imeweka wazi kwamba wanahitaji huduma ya supastaa huyo wa Ufaransa, ambaye amekuwa akiishabikia miamba hiyo ya La Liga tangu utoto wake.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez na bodi yake ya wakurugenzi wana uhakika mkubwa wa kunasa saini ya Mbappe kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, kisha mwakani itafanya mchakato wa kumsajili Erling Haaland.
Inaelezwa ni kwamba Borussia Dortmund imeweka kipengele cha Haaland kuuzwa kwa Pauni 63 milioni tu itakapofika mwakani, hivyo miamba hiyo ya Bernabeu inaamini itashinda kwenye mchakato wa kunasa huduma ya mshambuliaji huyo kwa kuwa mwenyewe anataka kwenda kuvaa jezi za Los Blancos.
Real Madrid mpango wao ni kumfanya Haaland kwenda kuwa pacha wa Mbappe kwenye fowadi ya timu hiyo ya Bernabeu wakati itakapounda Galacticos mpya. Ishu ya Mbappe itamaliza mwaka huu na Haaland mwakani.
Liverpool nao wamekuwa wakihusishwa na Mbappe, ambapo mchezaji huyo amekuwa na heshima kubwa kwa kocha wa miamba hiyo ya Anfield, Jurgen Klopp.
Lakini, kwa hali ilivyo kwa sasa, Real Madrid ndio wenye nafasi kubwa ya kunasa huduma ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2018 baada ya mchezaji mwenyewe kuonekana kuweka milango wazi ya kutua Bernabeu.