Barcelona yampa pigo Rashford
Muktasari:
- Adeyemi mwenye miaka 24 anayefunga na kucheza pembeni anakuwa usajili wa pili wa Barcelona majira haya ya kiangazi baada ya Anthony Gordon kuwasili kutoka Newcastle.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi, kwa ada inayoweza kufikia euro milioni 31 (pauni milioni 26.5).
Adeyemi mwenye miaka 24 anayefunga na kucheza pembeni anakuwa usajili wa pili wa Barcelona majira haya ya kiangazi baada ya Anthony Gordon kuwasili kutoka Newcastle.
Katika mechi 146 alizoichezea Dortmund alifunga mabao 36 na kutoa asisti 25, ingawa mara nyingi alikosolewa kwa kushindwa kudumu katika kiwango bora.
Adeyemi sasa ataungana tena na kocha Hansi Flick, aliyempa nafasi ya kwanza katika timu ya taifa ya Ujerumani.
Usajili huo ni pigo kwa Marcus Rashford, ambaye alikuwa akitarajia Barcelona ifanye uhamisho wake wa mkopo kuwa wa kudumu baada ya kufanya vizuri msimu uliopita.
Barcelona ilikuwa na nafasi ya kumsajili Rashford kwa pauni milioni 26 mwezi Juni baada ya kuchangia mabao 14 na asisti 14 katika mechi 26 alizoanza.
Badala yake wakaamua kumsajili Anthony Gordon wakiamini ana uwezo mkubwa zaidi wa kusaidia kazi za kujihami.
Kwa sasa Rashford anahusishwa na Arsenal, Tottenham na Real Madrid lakini hatma yake bado haijafahamika.
Baada ya mapumziko ya Kombe la Dunia anatarajiwa kurejea Manchester United kwa maandalizi ya msimu mpya na kuna uwezekano akaunganishwa tena katika kikosi cha kwanza chini ya Michael Carrick.
Msimu uliopita Adeyemi aliwahi kutozwa faini ya euro 450,000 kwa kukutwa na silaha haramu ikiwemo knuckle-duster na taser.
Baadaye aliomba radhi hadharani akisema lilikuwa kosa kubwa ambalo limemfundisha mengi.
Baada ya kutambulishwa Barcelona amesema:
"Kwa kweli sikuamini kama dili hili lingetokea kwa sababu najua msimu uliopita haukuwa bora kwangu."
"Ninamshukuru Hansi Flick kwa kuniamini na kuniambia ananihitaji."
"Nina heshima kubwa na nafasi hii."
Adeyemi amesaini mkataba wa miaka mitano na Barcelona.