Mbappe aangushiwa jumba bovu Madrid
Muktasari:
- Real Madrid ilitolewa kwenye hatua ya robo fainali na Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-4 katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa na pia iliyojaa matukio ya utata.
PARIS, UFARANSA: MAMBO magumu, ndivyo unavyoweza kusema! Nyota wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Emmanuel Petit amemkosoa straika Kylian Mbappe akidai amepeleka ubinafsi ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha Real Madrid kufuatia timu hiyo kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Real Madrid ilitolewa kwenye hatua ya robo fainali na Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-4 katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa na pia iliyojaa matukio ya utata.
Petit ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka nchini Ufaransa, alisema kuwa kuwasili kwa Mbappe Real Madrid kulipeleka mabadiliko mabaya katika mshikamano wa timu hiyo.
“Si kwamba yote ni kosa la Mbappé pekee,” alisema Petit na kuongeza:
“Lakini kuwasili kwake kumejaza ubinafsi ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha Real Madrid. Hii imekuwa kama janga.”
Aliongeza kuwa wakati Mbappehakuwepo kwenye kikosi cha kwanza kwa muda mfupi kutokana na majeraha, Real Madrid walionekana kucheza kwa pamoja zaidi na kupata matokeo mazuri, ikiwa ni pamoja na ushindi dhidi ya Manchester City na Atletico Madrid.
Hata hivyo, baada ya kurejea kwake, timu hiyo imepata matokeo mabaya mfululizo, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa nchini Hispania na Ulaya kwa ujumla.
Petit pia alisifu Paris Saint-Germain (PSG), klabu ya zamani ya Mbappé, akisema imekuwa bora zaidi tangu nyota huyo alipoondoka 2024.
“Kipindi ambacho Mbappé aliondoka PSG, sasa wanaonekana kuwa timu moja yenye mshikamano mkubwa. Wamekuwa bora sana,” alisema.
Kabla ya mechi za wikiendi hii, msimu huu wa 2025/26, Mbappe amefunga mabao 23 katika Ligi ya Hispania na kutoa asisti nne huku akifunga mabao 15 na kutoa asisti moja katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, Petit alikiri kuwa kufungwa kwa Real Madrid hakutokana na Mbappé pekee, akimtaja kiungo Eduardo Camavinga kama mmoja wa waliochangia zaidi kutokana na kadi nyekundu aliyopata.
“Makosa makubwa yalitokea kwa Camavinga. Kadi yake nyekundu ilikuwa na madhara makubwa sana kwa timu,” aliongeza Petit.
Baada ya mchezo huo, kulikuwa na mvutano mkubwa kwa upande wa Real Madrid, ambapo baadhi ya wachezaji walimlalamikia mwamuzi Slavko Vincic huku Arda Guler na wengine wakionekana kupinga maamuzi hayo kwa hasira.
Kocha wa Real Madrid, Álvaro Arbeloa pia alieleza kuwa timu yake ilistahili zaidi, lakini akakiri kuwa kadi nyekundu ilibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo huo.
Kwa sasa mjadala mkubwa unaendelea kuhusu hali ya ndani katika chumba cha kubadilishia nguo kwenye kikosi cha Real Madrid na nafasi ya Mbappé katika timu hiyo, huku mashabiki wakigawanyika juu ya lawama hizo.