Mastaa watano Celta Vigo kuinogesha mechi yao na Barca
Muktasari:
- Barcelona inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na shinikizo kubwa la kushinda ili kuendelea kuifukuzia Real Madrid kileleni, huku Celta Vigo ikiwa na rekodi nzuri ya nyumbani dhidi ya wababe hao wa Catalonia.
Wachezaji watano wa zamani wa Barcelona, wanaweza kuanza dhidi ya klabu hiyo leo Jumapili, Novemba 9, 2025, wakati Celta Vigo itakapokabiliana na FC Barcelona kwenye uwanja wa Balaídos, ikiwa ni mechi ya La Liga.
Barcelona inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na shinikizo kubwa la kushinda ili kuendelea kuifukuzia Real Madrid kileleni, huku Celta Vigo ikiwa na rekodi nzuri ya nyumbani dhidi ya wababe hao wa Catalonia.
Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, kuna mvuto wa kipekee katika mechi hiyo kwani wachezaji hadi watano waliowahi kuwa sehemu ya Barcelona wanaweza kuanza wakiwa upande wa Celta Vigo leo usiku.
Wachezaji hao ni Óscar Mingueza, Marcos Alonso, Ferran Jutglà, Ilaix Moriba na Marc Vidal, ambao waliwahi kuwa sehemu ya klabu ya Barcelona kwa nyakati tofauti na sasa ni wachezaji wa kikosi cha Celta.
Barcelona bado inamiliki asilimia 50 ya haki za Mingueza, pamoja na kipengele cha kumnunua tena (buy-back clause). Mchezaji huyo aliyelelewa katika kituo cha La Masia ameendelea vizuri tangu aondoke.
Kwa upande mwingine, Marc Vidal ana uwezekano mdogo wa kuanza, kwani yeye ni kipa wa akiba wa Celta Vigo. Hakuchezea kwenye timu ya kwanza ya Barcelona na ndiye mwenye jina dogo zaidi kwenye orodha hiyo.
Jutglà na Moriba wote walipitia akademi ya Barcelona. Jutglà alipata nafasi chache tu kwenye kikosi cha kwanza kabla ya kuhamia Club Brugge, ambako aliimarika, na kisha Celta Vigo ikamrudisha Hispania msimu huu.
Moriba, alikuwa mmoja wa vipaji vinavyoahidi sana katika kituo cha La Masia, lakini uamuzi wake ya kuondoka kuelekea RB Leipzig ulizua utata. Marcos Alonso naye alijiunga na Barcelona akitokea Chelsea kwa uhamisho huru na akacheza misimu michache.
Mambo haya yote yanaongeza mvuto zaidi kwenye mechi ya leo, na mashabiki wanatarajia kuona kama Barcelona itaweza kuondoka na pointi tatu muhimu.