Barcelona yamchukiza Henry, amkosoa Hansi Flick
Muktasari:
- Kikosi cha Catalunya kilifanikiwa kupata sare hiyo nchini Ubelgiji, lakini mashabiki wake waliibua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa kufika mbali kwenye mashindano hayo msimu huu, baada ya safu yao ya ulinzi kuonekana dhaifu tena.
Nyota wa zamani wa Barcelona, Thierry Henry, amemkosoa kocha wa sasa wa klabu hiyo, Hansi Flick, baada ya kikosi chake kulazimisha sare ya mabao 3–3 dhidi ya Club Brugge katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, jana Jumatano, Novemba 5, 2025.
Kikosi cha Catalunya kilifanikiwa kupata sare hiyo nchini Ubelgiji, lakini mashabiki wake waliibua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa kufika mbali kwenye mashindano hayo msimu huu, baada ya safu yao ya ulinzi kuonekana dhaifu tena.
Henry ambaye aliitumikia Barcelona kuanzia mwaka 2007 hadi 2010, amesema kocha Flick ana kazi kubwa ya kufanya ili kuwaaminisha mashabiki kuwa, kikosi chake kina uwezo wa kupambana na kufikia malengo msimu huu.
Amesema ni aibu kuona Barcelona inashindwa kuwa na safu nzuri ya ulinzi, hali ambayo inawavunja nguvu wachezaji wengine ambao wanaonekana kujituma wakati wote kwa kuisaidia timu kupata matokeo mazuri.
“Sitaki kuzungumza vibaya kuhusu klabu yangu ya zamani, lakini ni lazima tuwe wakweli,” ameiambia CBS Sports.
“Huwezi kuendelea kujilinda kwa namna hii. Kwa kweli sijawahi kuona Barcelona inayocheza kwa uadhaifu kama hii, safu ya ulinzi imeonekana kutokuwa makini sana, hali hii inawavunja nguvu wachezaji wengine ambao wanapambana kuipigania timu wakati wote, kwa hili kocha anapaswa kutafuta mbinu mbadala ili kuinusuru timu hii kupata aibu!” amesema Henry ambeya alifunga mabao 49 akiwa na Barca.
Licha ya ukosoaji huo, Hansi Flick alionekana kutotaka kubadili mbinu zake baada ya mchezo huo, kwa kusema: “Tunaweza kubadilisha baadhi ya mambo, lakini tunapaswa pia kushikilia falsafa yetu. Hatuhitaji kubadilisha mtindo wetu wa uchezaji, sisi ni Barça.”