Mastaa Liverpool mazoezini bila Jota
Muktasari:
- Mastaa wa Liverpool akiwamo Mohamed Salah, Andrew Robertson na usajili wao mpya, Jeremie Frimpong walipigwa picha wakiwa kwenye magari yao wakiwasili kwenye siku ya kwanza ya mazoezi huku klabu hiyo ikiendelea kuomboleza msiba.
LIVERPOOL, ENGLAND: HAKUNA namna, maisha lazima yaendelee. Ndicho unachoweza kusema baada ya mastaa wa Liverpool kurejea mazoezini huko Kirkby, Jumanne asubuhi ikiwa ni saa 72 tu tangu walipotoka kuhudhuria maziko ya mchezaji mwenzao, Diogo Jota nchini Ureno.
Mastaa wa Liverpool akiwamo Mohamed Salah, Andrew Robertson na usajili wao mpya, Jeremie Frimpong walipigwa picha wakiwa kwenye magari yao wakiwasili kwenye siku ya kwanza ya mazoezi huku klabu hiyo ikiendelea kuomboleza msiba.
Jota, 28, na mdogo wake Andre Silva, 26, walifariki dunia asubuhi ya Alhamisi baada ya gari waliyokuwa wakisafiria Lamborghini kupasuka tairi na kuwaka moto wakiwa huko Hispania walipokuwa wakiwahi kivuko cha kuwafikisha Portsmouth, England.
Kifo cha Jota na mdogo wake kilishtua dunia ya wapenda soka na kutuma salamu zao za pole.
Mo Salah alikiri kwenye posti yake aliyotuma mtandaoni itampa wakati mgumu sana kuona Jota hatakuwamo kwenye orodha ya wachezaji watakaorudi kwenye timu hiyo kujiandaa na msimu ujao.
“Ukweli nimeishiwa maneno,” aliandika Mo Salah.
“Hadi sasa, nilikuwa siamini kama kuna kitu kitaniweka kwenye wakati mgumu wakati nitakaporudi Liverpool baada ya mapumziko kumalizika. Wachezaji wanakuja na kuondoka, lakini si kwa staili hii. Ni ngumu sana kukubali Diogo hatakuwapo wakati tutakaporudi mazozini.”
Kocha mkuu wa Liverpool, Arne Slot alisema mshtuko ni kitu cha kawaida huku akiongeza, Jota alikuwa kipenzi cha kila mtu huko Anfield.
Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp, ambaye alimsajili Jota huko Anfield mwaka 2020, aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram : “Hizi ndizo nyakati zinazonipa wakati mgumu. Kuna kusudio kubwa la Mungu, lakini mimi siwezi kuliona. Moyo wangu umevunjika kwa niliposikia kifo cha Diogo na mdogo wake Andre. Diogo si tu alikuwa mchezaji mahiri, lakini pia ni rafiki mzuri, ana upendo na mume anayejali na pia ni baba. Tutamkumbuka sana. Sala zangu zote kwa Rute, watoto, familia na marafiki na kila mtu aliyekuwa na upendo kwake. Pumzika kwa amani – Love J.”
Beki wa pembeni, Andy Robertson, ambaye alihudhuria maziko yaliyofanyika Gondomar, alisema: “Ninachofikiria kwa sasa ni familia yake. Machungu yake ni magumu sana kuyahimili. Huzuni sana tumepoteza mioyo miwili iliyosafi kabisa Diogo na Andre.”
Na straika wa Liverpool, Darwin Nunez aliongeza: “Hakuna maneno yanayotosha kwenye maumivu makali. Siku zote nitakukumbuka kwa tabasamu lako na ule msaada wako ndani na nje ya uwanja.”
Liverpool mechi yake ya kwanza ya kirafiki imepanga kucheza na Preston North End huko Deepdale, Jumapili hii.
Lakini, uamuzi wa mechi hiyo kama itafanyika au kutofanyika itafahamika baada ya Kocha Arne Slot kuzungumza na wachezaji wake kwanza.