Mashabiki wa Man City kupata makazi ya kifahari Abu Dhabi
Muktasari:
- Klabu hiyo ya Ligi Kuu England, ambayo zamani ilipewa jina la utani la “majirani wenye makelele” na aliyekuwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, inatarajia kuwa na mradi wake wa kwanza wa makazi nchini humo.
ABU DHABI, UAE: MASHABIKI wa Manchester City wenye uwezo wa kifedha sasa wanaweza kuishi katika makazi ya kifahari yenye mandhari na utamaduni wa klabu hiyo katika mji wa Abu Dhabi, nchi ambayo wamiliki wa klabu hiyo wanatoka.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu England, ambayo zamani ilipewa jina la utani la “majirani wenye makelele” na aliyekuwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, inatarajia kuwa na mradi wake wa kwanza wa makazi nchini humo.
Mradi huo unaojengwa kando ya Yas Canal, utakuwa na mchanganyiko wa vyumba vya kifahari, majengo ya ghorofa, nyumba za kawaida na majengo ya kifahari yenye vyumba kati ya kimoja na vitano.
Bei ya nyumba hizo inaanzia takribani pauni 350,000 na kwa baadhi ya nyumba za kifahari inaweza kufikia karibu pauni6 milioni.
Wakazi pia watapata fursa ya kutumia kituo cha michezo chenye msukumo wa Manchester City, kitakachojumuisha viwanja vya soka vilivyo juu ya majengo pamoja na vyumba maalumu vya kuchambua mbinu za mchezo.
Kwa mashabiki wenye ndoto za kuwa nyota wa soka, kutakuwa pia na fursa ya kujiunga na akademia ya soka, ambapo wanaweza kujifunza na kuendeleza vipaji vyao wakitamani kufuata nyayo za mastaa wa City kama Erling Haaland na Phil Foden.
Mradi huo mkubwa unatarajiwa kuwa na zaidi ya nyumba 2,000, ukiundwa kama mji mdogo wa kisasa wenye huduma mbalimbali kwa wakazi wake.
Kituo kikubwa cha mazoezi chenye teknolojia za kisasa kitakuwa sehemu ya huduma zitakazopatikana katika eneo hilo.
Wakazi pia watakuwa na ufukwe wao binafsi pamoja na lagoon bandia, huku mashabiki wa City wakipewa eneo maalumu litakalojulikana kama City Social Club.
Pia, kutakuwa na maeneo maalumu ya kutazama mechi wakati wa siku za michezo, yakilenga kuwapa wakazi mazingira ya kushangilia timu yao wakiwa pamoja.
Mradi huo pia utakuwa na migahawa ya kiwango cha juu, klabu ya michezo ya majini na mabwawa ya kuogelea yaliyo juu ya majengo.
Msanidi wa mradi huo, Ohana, ambao bado wanaendelea na ujenzi, wameuelezea kama “mahali ambapo ubora wa soka unakutana na anasa ya maisha ya ufukweni.”
Hivyo, kwa mashabiki wa Manchester City wenye uwezo wa kumudu gharama hizo, ndoto ya kuishi katika mazingira yanayohusishwa moja kwa moja na klabu yao sasa inakaribia kuwa kweli.