Martinelli aingia anga za Madrid, bei yatajwa
Muktasari:
- Madrid ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga, inaamini Martinelli anaweza akasaidia kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo halionekani kufanya vizuri kwa sasa.
RIPOTI zinafichua Real Madrid imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Martinelli, katika harakati za kuboresha safu yao ya ushambuliaji, inaelezwa.
Madrid ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga, inaamini Martinelli anaweza akasaidia kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo halionekani kufanya vizuri kwa sasa.
Vigogo hawa wa Hispania, wamekuwa na panda shuka nyingi tangu kuanza kwa msimu huu na sasa imepoteza mechi mbili mfululizo moja ikiwa ni ile ya Spanish Super Cup mbele ya mahasimu wao Barcelona iliyosababisha Kocha Xabi Alonso kufukuzwa kazi.
Ripoti zinadai Arsenal ipo tayari kumuuza lakini inahitaji kiasi kisichopungua Euro 100 milioni kutokana na umuhimu wa fundi huyu katika kikosi chao.
Kiasi hicho cha pesa kinaonekana kuwa huenda kikachelewesha dili ingawa kunaweza kufanyika mazungumzo ya kuona jinsi ya kukipunguza.
Mkataba wake wa sasa na Arsenal unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote na kufunga mabao tisa.
Huyu sio mchezaji wa kwanza wa Arsenal kuhusishwa na Madrid katika miaka ya hivi karibuni, aliwahi pia kuhusishwa Gabriel Magalhaes ambaye mwishowe aliamua kusaini mkataba wa kuendelea kuwatumikia washika mitutu hao.
Joao Gomes
MABOSI wa Atletico Madrid wameanza kufanya mazungumzo na Wolves kwa ajili ya kiungo wao na timu ya taifa ya Brazil, Joao Gomes, 24, baada ya klabu hiyo ya Hispania kumuuza kiungo wao raia wa England, Conor Gallagher, kwenda Tottenham wiki hii.
Gomes mwenyewe anaonekana kuwa tayari kujiunga na timu hiyo ya jijini Madrid akiamini ni sehemu ya kukua zaidi kisoka na Atletico wanamwona kama mbadala sahihi wa Gallagher katika mfumo wa Diego Simeone, ambaye anapendelea zaidi wachezaji wenye nguvu na uwezo mkubwa wa kukaba. Mkataba wa Gomes unatarajiwa kumalizika 2030.
Marshall Munetsi
KIUNGO wa Wolves na timu ya taifa ya Zimbabwe, Marshall Munetsi, 29, yupo karibu kujiunga na Paris FC kwa mkopo wa nusu msimu.
Munetsi amekuwa akihangaika kupata nafasi ya kudumu kikosi cha Wolves msimu huu, hali iliyomfanya kuangalia fursa ya kupata muda zaidi wa kucheza.
Paris FC wanaamini anaweza akawasaidia kwa sababu tayari ana uzoefu wa ligi hiyo alioupata akiwa anacheza Reims. Kabla ya kutua Reims, Munetsi alikuwa akicheza Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
...
Youssef En-Nesyri
EVERTON wametuma ofa rasmi kwa klabu ya Uturuki, Fenerbahce, kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Morocco, Youssef En-Nesyri, 28.
Mazungumzo yanaendelea na inaelezwa Everton inataka kumchukua kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua kwa Pauni 17 milioni mwisho wa msimu.
En-Nesyri anaonekana kuwa suluhisho la tatizo la mabao na mabosi wa Everton wamevutiwa sana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na Morocco katika michuano ya mataifa ya Afcon. Huduma ya En-Nesyri pia inahitajika na Nottingham Forest.
Callum Wilson
EVERTON inataka kumsajili mshambuliaji raia wa England, Callum Wilson, 33, ambaye kwa sasa yuko katika mazungumzo ya kuvunja mkataba wake na West Ham.
Wilson anataka kuondoka West Ham kwa sababu hapati nafasi ya kutosha na anafikiria kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Baadhi ya taarifa zinafichua mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa Ligi Kuu England anataka kuvunja mkataba wake na West Ham kwa sababu ana ofa kutoka Saudi Arabia.
Yukhym Konoplya
EVERTON, Werder Bremen na Ajax zote zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya beki wa kulia wa kimataifa wa Ukraine, Yukhym Konoplya, 26, ambaye mkataba wake na Shakhtar Donetsk unamalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Timu nyingi zinaonyesha kutaka kusubiri hadi mwisho wa msimu ili kumpata akiwa mchezaji huru lakini baadhi zinafikiria kutuma ofa ya kumsajili wakati huu.
Tangu kuanza kwa msimu huu, staa huu amecheza mechi 19 za michuano yote, amefunga mabao mawili na kutoa asisti nne.
Sidiki Cherif
CRYSTAL PALACE wapo katika mazungumzo na Angers ya Ligue 1, kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Ufaransa, Sidiki Cherif, mwenye umri wa miaka 19.
Cherif ni mchezaji anayeweza kucheza katikati kama mshambuliaji namba tisa pia pembeni kama winga na tangu kuanza ka msimu huu amecheza mechi 18 za michuano yote na kufunga mabao manne.
Mkataba wake wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Donyell Malen
ROMA imekubali kulipa ada ya mkopo ya Pauni 2 milioni kwa ajili ya mshambuliaji wa Aston Villa na timu ya taifa ya Uholanzi, Donyell Malen, 26, na katika makubaliano hayo kuna kipengele kinachoeleza Roma itamnunua mazima fundi huyu kwa Pauni 25 milioni ikiwa itavutiwa na kiwango chake.
Malen alijiunga na Aston Villa akiwa na matarajio makubwa, lakini amekuwa akikosa nafasi ya mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
Mabosi wa Roma wanamwona kama suluhisho muhimu la kuongeza mabao na kasi katika safu yao ya ushambuliaji, hasa katika michuano ya Serie A na kimataifa.
Alex Scott
BOURNEMOUTH inaamini kuwa itakutana na wakati mgumu katika mpango wa kutaka kumbakisha kiungo wao wa kimataifa wa England, Alex Scott, 22, kutokana na kundi kubwa la vigogo wa England ambao wanahitaji saini yake.
Staa huyu anahitajika sana na Manchester United, Manchester City, Aston Villa na Newcastle United ambazo bado zinafanya mazungumzo na wawakilishi wake na zinaweza kutuma ofa dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi.
Mabosi wa Bournemouth hawataki kumuuza fundi huyu na ikiwa itamuuza itahitaji kiasi kikubwa sana cha pesa.