Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maresca achafukwa Kombe la Dunia la Klabu

ENZO Pict

Muktasari:

  • Maresca alikasirishwa na jinsi mchezo wao ulivyositishwa katika dakika ya 86 kwa karibu saa mbili kutokana na radi kupiga hali hiyo iliwaacha wachezaji wakiwa hawafanyi chochote ili kuweka miili sawa ndani ya muda wote huo.

LONDON, ENGLAND: LICHA ya timu yake kupata ushindi na kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu, kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alikosoa mechi yao dhidi ya Benfica ya 16 bora akisema haikuwa mchezo wa mpira wa miguu bali ni kama kulikuwa na utani ndani yake baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya saa mbili kutokana na hali ya hewa.

Maresca alikasirishwa na jinsi mchezo wao ulivyositishwa katika dakika ya 86 kwa karibu saa mbili kutokana na radi kupiga hali hiyo iliwaacha wachezaji wakiwa hawafanyi chochote ili kuweka miili sawa ndani ya muda wote huo.

Chelsea ilikuwa ikidhibiti mchezo kwa muda wote kabla ya kusitishwa na iliporejea uwanjani, ilipoteza uongozi wao wa 1-0 kwa penalti  iliyofungwa na Angel Di Maria baada ya Malo Gusto kuonekana kuushika mpira kwa mkono katika eneo la boksi.

Hata hivyo, Chelsea iliweza kushinda 4-1 katika dakika 30 za muda wa nyongeza huku Benfica ikimpoteza Gianluca Prestianni kwa kadi ya pili ya njano.

“Kwa dakika 85, tulikuwa tunaudhibiti mchezo, hatukuruhusu chochote. Tulitengeneza nafasi za kutosha, lakini baada ya kusitishwa, mchezo ulibadilika kabisa. Kwangu binafsi, sioni kama tunacheza mpira, hadi muda huu kuna mechi saba hadi tisa zilizositishwa, nadhani kuna masihara, haifai kuwa hivi, kama zinasitishwa mechi saba au nane ina maana hili si eneo sahihi kwa ajili ya kuandaa mashindano haya.”

Chelsea itacheza dhidi ya Palmeiras katika robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu huko Philadelphia Ijumaa, katika mchezo ambao utawakutanisha na  kijana wao chipukizi mwenye umri wa miaka 18, Estevao Willian ambaye atajiunga nao baada ya kumalizika mashindano hayo.

Mechi nyingine zilizositishwa kutokana na hali mbaya ya hewa katika michuano hiyo inayofanyika Marekani ni Benfica dhidi ya Auckland City, Ulsan dhidi ya Mamelodi Sundowns zote zilipigwa jijini Orlando. Pia mechi nyingine ni kati ya Red Bull Salzburg dhidi ya Pachuca iliyopigwa Cincinnati, Boca Juniors dhidi ya Auckland City(Nashville), na Palmeiras dhidi ya Al Ahly (New Jersey).

Maresca aliendelea kusema: “Tatizo ni kwamba mchezo unapositishwa, si soka. Jamani, si soka. Ukisitisha mchezo, si soka. Ni kitu tofauti kabisa.

“Mchezo ulikuwa mzuri sana kwa dakika 85. Halafu tukawa na kusitishwa kwa saa mbili. Kisha ulianza tena tofauti kabisa, haukuwa vile tulivyokuwa tunacheza kabla, watu walikuwa wameshaanza kuzungumza na familia zao wakiwauliza kama wako salama, wengine walikuwa wanakula, wengine wanacheka, kwa sababu muda ulikuwa ni mwingi sana (wa mchezo kusimama.”