Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manchester United waambiwa... Kocha ni Ancelotti

CARLO Pict

Muktasari:

  • Kwa sasa kikosi hicho kinachoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kipo chini ya kocha wa muda, Michael Carrick.

RIO DE JANEIRO, BRAZIL: HUKO Old Trafford maswali yamekuwa mengi kuhusu sakata la kocha wa kudumu wa kuinoa Manchester United kuanzia msimu ujao.

Kwa sasa kikosi hicho kinachoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kipo chini ya kocha wa muda, Michael Carrick.

Wakati kukiwa na mgongano wa mawazo kuhusu Carrick kama apewe kibarua cha kudumu au la, kuna staa wa zamani wa Tottenham Hotspur na Real Madrid, ambaye aliwahi kuhusishwa sana na Man United, amewapa mchongo mabosi wa timu hiyo ni kocha gani wanayepaswa kumchukua.

Winga ghali aliyewahi kutokea kwenye soka, Gareth Bale amemtaja kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti kama chaguo bora la kuinoa Man United badala ya Carrick, akimwelezea Mtaliano huyo ni mtu mwenye akili nyingi kwenye soka.

Carrick kwa sasa amerejea Man United kama kocha wa muda hadi mwisho wa msimu. Tangu achukue nafasi hiyo, ameiongoza timu kushinda mechi sita kati ya nane alizosimamia. Lakini, baada ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Newcastle United, Jumatano, ambacho ni cha kwanza kwa Carrick tangu aanze kuiongoza timu hiyo, kumeibua upya wa nani anafaa na nani hafai kupewa kibarua cha kudumu Man United.

Mastaa kadhaa wa zamani wa timu hiyo wakiongozwa na Paul Scholes, Gary Neville na Roy Keane hawaungi mkono Carrick kupewa mikoba ya kudumu, wakiamini kwa hadhi ya timu kama Man United inahitaji kocha mkomavu na mwenye uzoefu wa kutosha.

Miongoni mwa majina yanayotajwa ni Carlo Ancelotti, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Brazil na anatarajiwa kuwaongoza katika Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika majira ya kiangazi mwaka huu huko Amerika Kaskazini.

Ancelotti mwenye umri wa miaka 66 ana uzoefu mkubwa wa kufundisha katika klabu kubwa duniani. Bale aliwahi kufanya kazi na Ancelotti wakati wa kipindi chake cha kwanza Real Madrid kuanzia 2013 hadi 2015 na nyota huyo wa Wales alimpongeza sana kocha wake wa zamani.

Bale amesema: “Yeye si meneja tu, pia ni kocha halisi na anaelewa sana masuala ya mbinu za mchezo. Wakati wa kipindi chake cha pili Real Madrid, mwanawe alikuwa kocha msaidizi na walifanya kazi kubwa zaidi katika mbinu, lakini nadhani tulikuwa na timu bora zaidi kipindi cha kwanza.”

Winga huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 85 milioni na Real Madrid mwaka 2013 aliongeza: “Popote Carlo atakapokwenda, atafanya kazi nzuri sana kwa sababu anajua jinsi ya kumfanya kila mtu kuwa sehemu ya mpango wake. Ukienda katika klabu kubwa yenye wachezaji wazuri kama Manchester United, hata kama hawafanyi vizuri wakati fulani, bado ana uwezo wa kuwafanya kuwa na kiwango bora.”

Bale aliongeza kuwa moja ya siri kubwa ya mafanikio ya Ancelotti ni kurahisisha mambo ndani ya timu, aliposema: “Utamwona sasa Michael Carrick ameanza kurahisisha mambo mengi ambayo kocha wa zamani alikuwa akifanya na matokeo yanaanza kuonekana. Hiyo ndiyo jiniazi ya Carlo, kupata ubora wa wachezaji na kufanya mambo yawe rahisi.”

Hata hivyo, swali kubwa ni kama Ancelotti atakubali kazi ya kuinoa Man United. Kocha huyo wa Italia aliwahi kusema wazi mwaka uliopita kama atarejea kufundisha klabu baada ya Brazil, basi klabu pekee atakayokubali ni Real Madrid.

Ukiweka kando Real Madrid, Ancelotti pia amewahi kufundisha klabu kubwa kama Everton, Napoli, Bayern Munich, Paris Saint-Germain, Chelsea, AC Milan, Juventus na Parma.

Hivyo bado haijulikani kama Man United itafanikiwa kumshawishi kocha huyo mwenye mafanikio makubwa kurejea tena kufundisha katika ngazi ya klabu. Kama mpango wa kumpata Ancelotti, kitu ambacho kinaungwa mkono na gwiji wa Man United, Scholes ukikwama, basi mabosi wanaweza kumfikiria Carrick endapo kama ataendelea kufanya vizuri kwenye kikosi hicho hadi mwisho wa msimu na kuipa timu hiyo tiketi ya kushiriki mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.